Kansela wa Ujerumani bi Angela Merkel ametangaza kung'atuka katika wadhifa wake mwaka 2021, baada ya chama anachokiongoza na washirika wake kufanya vibaya katika chaguzi mbali mabali za hivi karibuni.
"Sitagombea nafasi yoyote ya kisisasa pale muhula wangu utakapomalizika," Bi Merkel amewaambia waandishi wa habari hii leo jijini Berlin.

Bi Merkel amekuwa madarakani tangu mwaka 2005 na amesema pia hatagombea kuchaguliwa kukiongoza tena chama chake cha CDU kwenye uchaguzi wa mwezi Disemba. Mwanasiasa huyo ameshika hatamu za uongozi wa CDU toka mwaka 2000.
Chama cha CDU kilipoteza kura nyingi katika jimbo la Hesse, ikiwa ni mwendelezo wa kushuka kwa ushawishi wa chama hicho katika mioyo ya Wajerumani.
Japo CDU na washirika wao wa Social Democrats wanaendelea kuliongoza jimbo la Hesse, wamepoteza asilimia 10 ya ushawishi waliokuwa nao katika jimbo hilo kwenye uchaguzi uliopita.
Uchaguzi wa Hesse umekuja wiki mbili baada ya uchaguzi katika jimbo tajiri zaidi la Bavaria ambao CDU na washirika wao wa CSU walifanya vibaya katika uchaguzi wa viti vya ubunge.
Vyama vya upinzani kama Greens na chama cha mrengo wa kulia AfD wamekuwa wakiungwa mkono kwa kasi toka Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2017 ambapo ushawishi wa vyama vikuu vya mrengo wa kati ulipoanza kutetereka.
Chama kama AfD kimewekeza nguvu zake katika kupinga sera ya uhamiaji iliyostawishwa na Bi Merkel ambapo chini ya uongozi wake mamilioni ya wakimbizi kutoka nchi za Syria, Afghanistan, Iraq na kwengineko wamepatiwa hifadhi Ujerumani.
Angela MerkelHaki miliki ya pichaREUTERS
Image captionBi Merkel alishinda Uchaguzi Mkuu wa 2017 lakini ushawishi wake ulishuka kwa kiwango kikubwa
Bi Merkel amesema "anawajibika moja kwa moja" na matokeo mabaya yanayoendelea kupatikana, na kusema hatomchagua mrithi wake ndani ya chama katika uchaguzi wa mwezi Disemba.
Uamuzi wa Bi Markel unaoneka ni moja ya jitihada za kuwanyamazisha wakosoaji wake ndani ya chama na kurudisha imani ya Wajerumani kwa chama hicho kikongwe. Lakini ni dhahiri kuwa uamuzi huo ni turufu yake ya mwisho ya kusalia madarakani katika kipindi hiki ambapo anguko lake kisiasa halizuiliki.
Maisha yake ya kisiasa kwa siku zijazo yatategemea nani atamrithi uongozi wa chama. Kama mshirika wake wa dhati Annegret Kramp-Karrenbauer atashinda, basi makabidhiano ya madaraka yatatokea bila bughudha na uwezekano wa Merkel kusalia madarakani mpaka 2021 ni mkubwa.
Hata hivyo, Tai tayari wanamzunguka wakijiandaa kumdonoa mpaka wammalize. Mpinzani wake wa siku nyingi ndani ya chama Friedrich Merz ametangaza kugombea nafasi ya uongozi wa juu wa CDU. Endapo Bw Merz ama mpinzani yeyote wa Bi Merkel atashinda basi Ukansela wake utakuwa mgumu na yawezekana akalazimika kubwaga manyanga hata kabla ya 2021.
Bi Merkel hapo kabla amekuwa akisisitiza kuwa ili aiongoze Ujermani barabara inampasa akiongoze na chama chake pia. Ukweli wa kauli hiyo upo mbioni kuthibitika.
Mwandishi wa BBC jijini Berlin Jenny Hill anasema Bi Merkel alijitahidi kuwa na sura ya bashasha lakini kuna muda alionekana dhahiri akiwa na huzuni katika mkutano wake na wanahabari ambao ulikuwa wa kuagana ns siasa za Ujerumani.