Benki ya Dunia imeridhia kutoa Dola za Marekani Milioni 300 sawa na shilingi bilioni 680.5 kwa Tanzania kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa kuongeza ubora wa elimu ya sekondari, Ikulu ya Tanzania imeeleza.

Fedha hizo zinaokusudiwa kujenga vyumba vya madarasa, mabweni, maabara, nyumba za watumishi na kununua vifaa vya kufundishia.
Makubaliano hayo yamefikiwa hii leo baada mkutano wa Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia Kanda ya Afrika Dkt. Hafez Ghanem na Rais John Magufuli yaliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Ghanem amesema pamoja na kuridhia kutoa fedha za mradi huo, Benki hiyo inaendelea kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo nchini Tanzania yenye thamani ya Dola za Marekani Bilioni 5.2 sawa na zaidi ya shilingi Trilioni 13.
Makubaliano hayo yanafuta maamuzi ya awali ya uongozi wa benki hiyo ya kuzuia mkopo huo.
Chanzo cha kuaminika kutoka benki hiyo kiliiambia BBC Swahili Jamatano, Novemba 14 kuwa mkopo huo ulisitishwa kutokana na ukiukwaji wa haki za binaadamu nchini Tanzania.
Sababu kuu mbili za zuio hilo zilikuwa ni mosi, uamuzi wa Rais John Magufuli wa kuzuia wanafunzi wanaopata ujauzito kuendelea na masomo mara baada ya kujifungua.
Pili, maboresho ya Sheria ya Takwimu yaliyopitishwa na Bunge la Tanzania Septemba 10 ambapo pamoja na mengine, inakataza usambazaji wa takwimu zinazolenga kupinga, kupotosha au kukinzana na takwimu rasmi za serikali.
Adhabu ya kufanya hivyo ni faini ya Dola 6,000 au kwenda jela miaka mitatu.
Afisa huyo wa Benki hiyo pia aliithibitisha BBC kuwa safari zote rasmi za wafanyakazi wa Benki ya Dunia zimesitishwa kutokana na hofu ya kukamatwa na kushtakiwa watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja.
KikaoHaki miliki ya pichaIKULU TZ
Hata hivyo, benki hiyo ilisema itaendelea na majadiliano na serikali ya Tanzania.
"Tukishirikiana na wadau wengine tutaendelea kupigania haki ya wasichana kupata elimu kwa kujadiliana na serikali ya Tanzania," ilisema sehemu ya barua pepe ya Benki ya Dunia kwa BBC Swahili.
Haijafahamika ni makubaliano gani yaliyofikiwa mpaka sasa mkopo huo umekubaliwa kutoka. Hata hivyo, Rais Magufulia amesema pesa hizo "hazijafyekelewa mbali" kama baadhi ya watu "wasiotutakia mema walivyosema."
Rais Magufuli amenukuliwa akisema kuwa Ghanem amekwenda Tanzania kuthibitisha kuwa Benki ya Dunia haitaiacha nchi hiyo.
WoteHaki miliki ya pichaIKULU TZ
"Namshukuru Dkt. Hafez Ghanem na Benki ya Dunia kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya miradi ya Tanzania, hizo Dola Milioni 300 ambazo baadhi ya watu wasiotutakia mema walisema zimefyekelewa mbali, anasema zitaletwa, na pia Benki ya Dunia imetoa Dola Bilioni 5.2 ambazo zinafadhili miradi mbalimbali ya elimu, nishati, barabara, kilimo, afya na maji, ni miradi mikubwa na mingi.
Kwa hiyo amekuja kututhibitishia kuwa Benki ya Dunia haitatuacha." amesema Rais Magufuli.
Mazungumzo kati ya Magufuli na Ghanem yamehudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Nje Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Palamagamba Kabudi, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako, Waziri wa Afya Ummy Mwalimu na Mwakilishi wa Benki ya Dunia Tanzania Bi. Bella Bird.