Mwanamfalme Mohammed bin SalmanHaki miliki ya pichaREUTERS
Image captionMwanamfalme Mohammed bin Salman ameiombaMarekani kulinda uhusiano wa mataifa hayo mawili
Mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia Arabia mwanamfalme Mohammed bin Salman aliwaambia maafisa wa Marekani kwamba anamchukulia mwanahabari aliyeuawa, Jamal Khashoggi kama mshirika hatari wa kundi la kiislamu lenye itikadi kali.

Mwanamfalme Mohammed ameripotiwa kusema hayo katika mazungumzo yake ya simu na maafisa wa Ikulu ya Marekani baada ya kupotea kwa mwanahabari Jamal Khashoggi.
Saudia hata hivyo imekanusha ripoti hiyo iliyochapishwa katika magazeti ya Washington Post na New York Times.
Khashoggi, ni raia wa Saudi Arabia aliyekuwa mchangiaji wa makala maalum katika gazeti la Washington Post.
Alikuwa mkosoaji mkubwa wa utawala wa kifalme nchini Saudi Arabia.
Jamal KhashoggiHaki miliki ya pichaEPA

Mwili haujapatikana

Mwili wa mwanahabari huyo mpaka sasa haujapatikana huku mwendesha mashtaka wa Saudi Arabia akisema mauaji ya Khashoggi yalikuwa yamepangwa.
Huku hayo yakijiri mtoto wa kiume wa Jamal Khashoggi, Salah pamoja na familia yake wamewasili Marekani siku chache baada ya kukutana na Mwanamfalme Mohammed Bin Salman.
Katika taarifa iliyochapisha magazetini familia nya Khashoggi imekanusha madai kwamba Khashoggi alikua mwanachama wa kundi la Muslim Brotherhood.
Familia hiyo pia imeongeza kwamba yeye mwenyewe aliipinga madai hayo mara kadhaa katika miaka ya hivi karibuni.
"Jamal Khashoggi hakua mtu hatari kwa vyovyote. Madai hayo ni ya kushangaza sana," ilisema taarifa hiyo.
Salah,mtoto wa kiume wa Jamal Khashoggi alipokutana Mwanamfalme Mohammed Bin SalmanHaki miliki ya pichaEPA
Image captionSalah,mtoto wa kiume wa Jamal Khashoggi alipokutana Mwanamfalme Mohammed Bin Salman
Uchunguzi umebaini nini kufikia sasa?
Mpaka sasa hakuna makubaliono yaliyofikiwa kuhusu jinsi Khashoggi alivyofariki.
Aliingia katika ubalozi mdogo wa Saudia mjini Istanbul kushughulikia stakabadhi za kumwezesha kumuoa mchumba wake wa Uturuki, Hatice Cengiz.
Siku ya Jumatano Uturuki ilisema kuwa aliuawa alipoingia ndani ya ofisi za ubalozi huo na mwili wake kukatwa katika vipande "kulingana na utaratibu uliopangwa awali''.
Vyombo vya habari vya Uturuki viliwahi kuripoti kuwa Khashoggi aliteswa kabla ya kuuawa.
Hatice Cengiz, aliyekuwa mchumba wa Jamal KhashoggiHaki miliki ya pichaEPA
Image captionHatice Cengiz, aliyekuwa mchumba wa Jamal Khashoggi
Saudi Arabia imebadilisha kauli yake ya awali kuhusu mkasa wa kutoweka na kuuawa kwa Khashoggi.
Habari za kutoweka kwake zilipoangaziwa kwa mara ya kwanza Saudi Arabia ilisema kuwa Khashoggi alitoka ndani ya ubalozi wake mjini Istanbul akiwa hai.
Lakini baadaye ikakiri kuwa aliuawa na watu hatari waliyokuwa wanatekeleza uparesheni ya kikatili.
Kufikia sasa Saudia imewakamata washukiwa 18 ambao inasema watashtakiwa nchini humo.
Uturuki inataka washukiwa hao wafunguliwe mashtaka katika taifa hilo kwasababu uhalifu ulifanywa katika ardhi yake.
Jamal KhashoggiHaki miliki ya pichaAFP/GETTY
Uturuki imeilaumu wazi wazi Saudia kwa kuhusika na mauaji ya Khashoggi.
Wiki iliyopita Rais Recep Tayyip Erdogan alizungumza na mfalme Salman wa Saudi Arabia na kukubaliana kushirikiana na kwa uchunguzi.
Mataifa mengine yanasema nini?
Saudi Arabia imekosolewa vikali kufuatia mauaji hayo huku washirika wake wa karibu wakitaka kupewa majibu kuhusu mkasa huo.
Rais Trump amesema ''hajaridhika'' na kauli ya Saudia lakini hata hivyo hayuko tayari kuvuruga mkataba wa kuiuzia silaha taifa hilo.
Mwanamfalme Mohammed Bin Salman wa Saudi Arabia na Rais TrumpHaki miliki ya pichaANDAR ALGALOUD / SAUDI KINGDOM COUNCIL / HANDOUT
Image captionMwanamfalme Mohammed Bin Salman wa Saudi Arabia na Rais Trump wa Marekani
Siku ya Alhamisi waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo alisema taifa lake litaendelea kutathmini suala hilo kwa wiki kdhaa kabla ya kufanya kufanya maamuzi kuhusu hatua itakayoichukulia Saudia.
Wanaharakati nchini Marekani wamezindua ombi la kutaka jina la sehemu ya barabara iliyopo karibu na ubalozi wa Saudi Arabia mjini Washington igeuzwe kuwa bara bara ya Jamal Khashoggi.
Siku ya Jumatano waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian alisema mauaji ya Khashoggi yalikuwa uhalifu na ukatili mkubwa