Jumanne, msimu wa Ligi Kuu Bara 2018/19 ulihitimishwa ambapo kila timu ilivuna kile ilichopanda tangu mwanzo hadi mwisho wa msimu. Tumeona bingwa amepatikana na timu zilizoshuka daraja zimefahamika.

Kilichobaki sasa ni kujipanga kwa msimu ujao unaoanza wiki ya mwisho ya mwezi Agosti. Bingwa wa msimu huu ni Simba, ambayo imeweza kutetea taji lake, hivyo karata zake ilizichanga vizuri na kufikia malengo. Nyuma ya ubingwa huo wa Simba, kuna mengi ambayo yamechangia ambapo makala haya inayabainisha kwa uchache.


UWEKEZAJI
Msimu wa nyuma yake yaani 2017/18 wakati Simba inatwaa ubingwa wa ligi kuu, ilikuwa na kikosi imara ambacho kilionyesha ushindani mpaka kufikia ndoto zake. Msimu huu wa 2018/19 kikosi kilifanyiwa maboresho ambayo yalitumia gharama kubwa sana.

Imeelezwa kuwa kikosi cha msimu huu cha Simba kiliundwa kwa gharama zaidi ya Sh Bilioni 1.3 ya msimu wa nyuma yake fedha ambazo ni nyingi kuwekeza chini ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya klabu hiyo, Mohammed Dewji ‘Mo’ ambaye ndiye bosi mkubwa ndani ya Simba.

Uwekezaji huo umewasaidia kupata aina ya kikosi ambacho kina wapamba naji wa kimataifa hali iliyowafanya wawe na uwezo wa kupata matokeo mazuri hadi wametetea ubingwa wao.
KOCHA
Patrick Aussems bado anatoa somo kwa makocha wengi ambao wanafundisha hapa Bongo kwamba mwalimu bora ni yule anayeleta changamto na kupata matokeo kwenye mechi bila kujali aina ya timu anayocheza nayo.

Amekuwa bora na hilo linadhihirisha kufikia malengo ambayo alikuwa nayo. Katika msimu wake wa kwanza ameipa Simba ubingwa wa Ligi Kuu Bara na kuifikisha timu hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Pia ametwaa tuzo ya Kocha Bora wa Ligi Kuu Bara mara mbili, hii inazidi kutoa majibu kwamba ni kocha bora, muda wote amekuwa ni
kocha anayeamini katika mbinu kabla ya kuwavaa waamuzi hasa anapoona wameshindwa kusimamia sheria.

“Nawajua wachezaji wangu juhudi zao zilipojificha na namna ambavyo wana uwezo wa kufanya makubwa ila muda mwingine wamekuwa wakinishangaza hasa wanapocheza chini ya kiwango, nafurahi kutwaa ubingwa, ni hatua nzuri kwangu, timu na mashabiki,” anasema Aussems wakati alipoifanikisha Simba kutetea ubingwa.
WACHEZAJI
Aina ya wachezaji wa Simba ilikuwa ni wale ambao wanajituma na kufanya kila mchezaji kuwa tishio hasa kwa upande wa safu ya ushambuliaji na safu ya ulinzi kote kulikuwa na aina ya wachezaji makini.

Ukiangalia idadi ya washambuliaji ambao wamefunga mabao mengi wanatoka Simba, kinara wa utupiaji ni Meddie Kagere mwenye mabao 23, huku John Bocco akiwa nafasi ya nne akitupia mabao 16 na nafasi ya tano ipo kwa Emmanuel Okwi mwenye mabao 15.

Sehemu ya kiungo imekuwa bora muda wote ikiwa inasimamiwa na kipenzi cha mashabiki wa Simba, Jonas Mkude, Haruna Niyonzima na Clatous Chama ambao walikuwa wanauchezea mpira namna wanavyotaka na kuilisha safu yao ya ushambuliaji.

Sehemu ya ulinzi nayo imekuwa bora ikiwa chini ya nahodha msaidizi, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ ambaye Aussems amemuamini na amekuwa bora kwa Simba akiwa amecheza michezo 29 kabla ya mchezo wa jana. Safu hiyo ya ulinzi imeruhusu mabao 15.
LIGI YA MABINGWA
Kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu kumewapa morali wachezaji pamoja na viongozi kuona umuhimu wa kuitangaza nchi kimataifa hasa kwa mafanikio ambayo walifikia msimu huu kwa kutinga hatua ya robo fainali. Safari ziliwapa mzuka sana.

Simba walitambua kwamba hakuna namna nyingine ya wao kushiriki michuano hiyo kwa msimu ujao zaidi ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara, hivyo waliporejea baada ya kutolewa na TP Mazembe hatua hiyo, nahodha, John Bocco alisema watapambana kurejea tena msimu ujao.
MASHABIKI
Mtaji mkubwa wa timu hii umekuwa kwa mashabiki hasa wanapotoa hamasa na
kuishangilia timu yao ikiwa uwanjani, hali hiyo imefanya wawe tofauti kidogo msimu huu hasa kwenye michezo ya ligi ambayo walikuwa wakicheza tangu mwanzo.

Mfano mzuri msimu huu kwenye michezo ile ya ‘Kariakoo Derby’ ambayo iliwakutanisha na watani zao Yanga, mashabiki wa Simba walijitokeza kwa wingi kutoa sapoti hata kwenye mechi ambayo wao walikuwa wageni, hii ilitosha kuwapa hasira wachezaji na benchi la ufundi kuwapa zawadi mashabiki wao.

Mashabiki hawakuishia sehemu moja pekee, bali wapo ambao walikuwa wakiongozana na timu hata inapocheza nje ya Dar. Hilo nalo limechangia kuwarejeshea ubingwa msimu huu.

MALENGO
Ligi ilipoanza msimu huu, Simba kupitia ofisa habari wake, Haji Manara, iliweka wazi kabisa malengo makuu ni mawili ambayo ni kutetea ubingwa wa ligi na kutinga hatua ya makundi kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika. vyote hivyo wamefanikiwa.

Hivyo uongozi wa Simba pamoja na wachezaji bila kusahau benchi la ufundi walikuwa wanatambua malengo yao na walikuwa wakijikumbusha mara kwa mara mwisho wa siku yote yametimia.