Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akizungumza na Timu ya Jumuiya ya Watanzania wanaoishi Nje ya Nchi {Diaspora} Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watanzania Waoishi Nje ya Nchi maarufu {Diaspora} akiwa pia Mjumbe wa Kamati ya Biashara Tanzania Bwana Jonas Njao akimkabidhi Balozi Seif Barua za maombi yakutaka kuanzisha Mradi wa Ujenzi wa Daraja kati ya Miji ya Dar es salaam na Zanzibar.
Afisa Muandamizi wa Kampuni ya Maxtruder yenye Mastakimu yake Nchini Ujerumani Mhandisi Felix Von Lumburg akimkabidhi Balozi Seif baadhi ya michoro ya ramani ya Nyumba za bei nafuu zinazojengwa naq Kampuni hiyo.
Balozi Seif kati kati akiwa katika picha ya pamoja na Timu ya Jumuiya ya Watanzania wanaoishi Nje ya Nchi {Diaspora} mara baada ya mazungumzo yao. Picha na – OMPR – ZNZ.
Uongozi wa Jumuiya ya Watanzania Waoishi Nje ya Nchi maarufu {Diaspora} uko tayari kusimamia Ujenzi wa Daraja refu la kisasa lenye uwezo wa kuunganisha Miji Miwili ya Dar es salaam na ule wa Zanzibar katika harakati za kuimarisha Uchumi na Mawasiliano.
Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo akiwa pia Mjumbe wa Kamati ya Biashara Tanzania Bwana Jonas Njao akiiongoza Timu ya Wanajumuiya hiyo alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Bwana Jonas Njao alisema Diaspora imeanza harakati za Maandalizi ya kufanya utaratibu wa kuziomba Serikali zote Mbili za Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya Mapinduzi ya Zanzibar kuuridhia Mradi huo Mkubwa wa Kimataifa utakaoweza kupunguza kundi kubwa la ajira Nchini Tanzania.
Alisema Wataalamu pamoja na Wafadhili wa ujenzi wa Mradi huo wa Kiuchumi tayari wameshajitokeza na kinachosubiriwa kwao kwa sasa ni kukubalika kwa maombi ya Mradi ambao bado umekuwa adimu ndani ya Bara la Afrika.
Bwana Jonas Njao alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba fursa wanazozipata za kuwasiliana na Taasisi na Makampuni wanamozunguuka katika Mataifa tofauti Duniani zimelenga kutafuta nafasi za ajira zitakazosaidia kuimarisha ustawi wa Wananchi kutokana na vijana wao kujikomboa katika masuala ya ajira.
Naye Afisa Muandamizi wa Kampuni ya Maxtruder yenye Mastakimu yake Nchini Ujerumani Mhandisi Felix Von Lumburg alisema Uongozi wa Taasisi yake uko tayari kuwekeza Miradi ya Ujenzi wa Nyumba zenye bei nafuu kufuatia ushawishi mkubwa walioupata kutoka Jumuiya ya Watanzania wanaoishi Nje ya Nchi.
Mhandisi Lumburg alisema ujenzi wa Nyumba Moja yenye thamani ya Dola za Kimarekani Elfu 5,000 hutumia Masaa Mawili tuu kuunganisha kuta zake zilizotengenezwa kwa zege yenye kuzingatia kiwango madhubuti cha Kimataifa.
Alisema Uongozi wa Kampuni hiyo mbali ya kujikita katika Miradi tofauti kutokana na Taaluma kubwa ya Wahandisi wake lakini imeamua kulenga katika ujenzi wa Nyumba hizo ili kusaidia Jamii za Wanaadamu hasa wale wanaoishi wakiwa na kipato cha chini.
Afisa Muandamizi huyo wa Kampuni ya Maxtruder amemuhakikishia Balozi Seif kwamba nyumba zinazojengwa na Kampuni hiyo zinahimili matukio ya dharura ikiwemo mitetemeko na tayari wameshajenga moja ya Mfano Nchini Kenya na mradi kama huo kwa sasa upo Nchini Russia.
Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Serikali zote Mbili Nchini Tanzania zimetoa fursa kwa Wananchi wake kutafuta Maisha mahali popote mali ilimradi wanazingatia Sheria na Taratibu za Mataifa wanaamua kuishi.
Balozi Seif alisema ni vyema kwa Watanzania hao walioko Ughaibuni wakachuma katika njia ya halali, wakala, lakini wasisahau kuweka hakiba kwa ajili ya kusaidia Familia zao pamoja na wao wenyewe.
Aliwaomba kuitumia fursa ya Uwekezaji iliyopo Nchini hivi sasa kwa kuanzisha Miradi ya uzalishaji vikiwemo viwanda vidogo na hata vikubwa ili vije kuwasaidia pale watakapoamua kurudi kumaliza maisha yao nyumbani.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwahakikishia Watanzania hao wanaoishi Ughaibuniu kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa vile tayari imesharidhia uwepo wa Jumuiya hiyo iko tayari kuwasaidia wana Diaspora hao kwa wale watakaoamua kuwekeza Miradi yao ikiwemo Nyumba na Mashamba.
Akigusia mradi wa Ujenzi wa Nyumba za bei nafuu Balozi Seif aliipongeza Kampuni ya Maxtruder kwa uamuzi wake iliyochukuwa ya kutaka kufungua Milango ya Uwekezaji katika Mataifa machanga yanayohitaji huduma hizo muhimu kwa ustawi wa Jamii.
Balozi Seif alisema Zanzibar ni miongoni mwa Nchi zenye maeneo madogo ya Ardhi. Hivyo aliushauri Uongozi wa Kapuni hiyo kuandika maombi yake yakutaka kuanzisha Miradi ya Ujenzi wa Nyumba.
0 Comments