Jarida la Forbes limemtangaza mwanamuziki maarufu duniani na mfanyabiashara Robyn Rihanna Fenty ‘Rihanna’ kuwa mwanamuziki wa kike milionea zaidi duniani akiwabwaga mastaa wenzake kama Madonna, Celine Dion na Beyonce.
Taarifa ya Jarida hilo iliyotoka jana imesema Rihanna ameshika nafasi ya kwanza akiwa na utajiri wa dola za Marekani milioni 600 ambao ni wastani wa Tsh trilioni 1.38.
Nafasi ya pili imeshikwa na Mwanamuziki Mkongwe, Madonna mwenye utajiri wa USD Milioni 570 (Tsh. Trilioni 1.31), nafasi ya tatu imeshikwa na Mkongwe mwingine, Céline Dion mwenye utajiri wa USD Milioni 450 (Tsh. Trilioni 1,03) huku nafasi ya nne ikishikwa na Beyoncé na utajiri wa USD Milioni 400 (Tsh. Milioni 919.04).
Utajiri mkubwa wa Rihanna unaripotiwa kutokana na kuingia ubia na Kampuni ya ‘French Luxury Goods Behemoth-LVMH’ inayoendeshwa na Bilionea, Bernard Arnault ambapo kwa pamoja wanamiliki Kampuni ya ‘Fenty Beauty‘ inayojishughulisha na kutengeneza vipodozi.
Staa huyo wa nyimbo Umbrella, Wild Thoughts, Rude Boy, Take a Bow na nyingine nyingi alianzisha kampuni ya vipodozi ya Fenty mwaka 2017 ambayo ilimuingizia dola za Marekani 100 (Tsh. Milioni 229.76) katika wiki ya kwanza ya mauzo. Mpaka mwishoni mwa mwaka jana, 2018, Kampuni ya Fenty Beauty anayoimiliki kwa asilimia 15, iliingiza jumla ya USD Milioni 570 (Tsh. Trilioni 1.31).
Forbes imeeleza kuwa utajiri mwingine wa Mwanamuziki huyo unatokana na umiliki wake wa pamoja na Kampuni ya nguo ya ‘TechStyle Fashion Group‘ katika nguo za ndani za ‘Savage X Fenty‘, lakini pia fedha nyingine zinatokana na kuachia nyimbo zake na kufanya matamasha ya muziki.
0 Comments