Klabu ya Brighton inayocheza ligi ya Primia ya England inaongoza msururu wa klabu zinazomuwania mshambuliaji wa Tanzania, Mbwana Samatta.
Klabu nyengine za England ambazo zinamuwania Samatta ni Aston Villa, Watford, Leicester na Burnley.
Kwa mujibu wa gazeti la The Sun la Uingereza Samatta ana thamani ya Pauni milioni 12.
Samatta ambaye bado ana mwaka mmoja kwenye mkataba wake na mabingwa wa Ubelgiji KRC Genk pia amezivutia klabu za Roma ya Italia na Lyon ya Ufaransa.
Mshambuliaji huyo ambaye aliongoza kwa kupachika mabao msimu uliopita nchini Ubelgiji ameweka wazi kuwa anataka kuelekea nchini England msimu ujao.
"Kwa sasa hivi siwezi kusema sana, ni kitu ambacho kipo kwenye mchakato nasubiria kitakapokuwa tayari na wakati utakapofika nitaweza kukizungumza. Lakini sijioni tena Genk, namuomba Mwenyezi Mungu litimie, lakini ikishindikana bado nina mkataba na Genk," aliiambia runinga ya Azam TV ya Tanzania wiki iliyopita.
Klabu ya Brighton imekuwa ikimfuatilia Samatta kwa muda mrefu na kocha wa timu hiyo kwa msimu uliopita Chris Hughton alikuwa akivutiwa sana na mchezaji huyo.
Kocha mpya wa klabu hiyo Graham Potter pia anavutiwa na uwezo wa Samatta.
Samatta ambaye pia ni nahodha wa Tanzania kwa sasa yupo kambini na timu ya taifa lake wakijiandaa na michuano ya bara la Africa (Afcon 2019) yatakayofanyika nchini Misri baadae mwezi huu.
Samatta ameliongoza taifa lake kwenda Afcon baada ya kukosa kwa miongo minne.
Samatta alijiunga na Genk akitokea TP Mazembe Januari 2016 ambapo alitia saini mkataba wa kumuweka katika klabu hiyo hadi msimu wa 2019/20.
Msimu uliopita, 2018/19 bila ya shaka ulikuwa bora kabisa kwake toka alipojiunga na klabu hiyo.
Amefunga magoli 23 ya ligi na magoli 9 kwenye michuano ya ligi ya Europa. Pia amepata tuzo ya Ebony ambayo hutuzwa mchezaji bora mwenye asili ya Afrika nchini Ubelgiji.
Pia ametoa mchango mkubwa kwa klabu hiyo kuchukua ubingwa wa ligi baada ya kuukosa kwa miaka minane.
Samatta alianza Maisha yake ya soka akiwa kinda na klabu ya Mbagala Market kisha akasajiliwa na Simba zote za Dar es Salaam Tanzania. Mazembe walimsajili 2011 akitokea Simba.
0 Comments