Watanzania ambao hawatakuwa wamepata pasipoti za kielektroniki kufikia mwisho wa mwezi huu hawataruhusiwa kusafiri nje ya nchi.
Kulingana na taarifa iliotolewa na msemaji wa idara ya uhamiaji Ally Mtanda matumizi yote ya pasipoti za zamani yatasitishwa kufikia tarehe 31 mwezi Januari 2020.

Hatua hiyo itawakwaza wale wote wanaotaka kusifiri nje ya nchi kwa kuwa hati za kusafiria zinahitaji kuwa na uhai wa angalau miezi sita ili mwenye hati hiyo aweze kuomba visa ya kwenda nchi nyingine.
Aidha idara hiyo imewasisitizia wale wote wenye pasipoti za zamani na wanaokusudia kusafiri nje ya nchi hivi karibuni kuhakikisha wanabadili pasipoti zao mapema kabla ya mwezi Julai mwaka huu ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza wa kurejeshwa katika viwanja vya ndege na vituo vya mpakani wakati wa kutoka nchini.
Hatua hiyo inajiri baada ya rais wa Tanzania Dkt John Magufuli kuzindua mfumo wa uhamiaji wa kutumia mtandao ambao unahusisha kutolewa kwa pasipoti za kielektroniki Tanzania.
Dkt Magufuli alisema hatua hiyo itasaidia kuimarisha ulinzi na usalama wa mipaka ya nchi na kusaidia kudhibiti ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali na kuimarisha utoaji wa huduma za kiuhamiaji kwa raia wa Tanzania na wageni wanaoingia na kuishi hapa nchini humo.
Kiongozi huyo alisema matumizi ya pasipoti mpya za kielektroniki, yataondoa matumizi ya pasipoti za kawaida zinazotumika sasa.
Rais Magufuli alisema pasipoti za kisasa zitakazotolewa zinakidhi viwango vya kimataifa kwa kuwa zina alama nyingi za kiusalama, na siyo rahisi kuzighushi licha ya gharama yake kutokuwa kubwa.
Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan na pasipoti yake mpya ya kielektronikiaHaki miliki ya pichaIKULU, TANZANIA
Uzinduzi wa mfumo huo ulifanyika katika ofisi kuu ya uhamiaji jijini Dar es salaam Jumatano.
Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Makakala amesema mfumo huo ni muunganiko wa mifumo mbalimbali ambayo imesanifiwa kufanya kazi kwa pamoja, kutoa taarifa kwa watumiaji na wadau wa huduma za kiuhamiaji.
Dkt Makakala amesema kwamba kupitia mfumo huo idara ya uhamiaji inatarajia kutoa pasipoti za kielektronikia (e-Passport), viza za kielektronikia (e-Visa), vibali vya ukaazi vya kielektronikia (e-Permit) na udhibiti wa mipaka wa kielektronikia (e-Border Management) kwa awamu nne hadi ifikapo mwisho wa mwaka huu 2018, pamoja na kutoa pasipoti ya kielektronikia ya Afrika Mashariki ya Tanzania.
  • Mfumo wa Uhamiaji wa Mtandao unashirikisha:
  • pasipoti za kielektronikia (e-Passport)
  • viza za kielektronikia (e-Visa)
  • vibali vya ukaazi vya kielektronikia (e-Permit)
  • udhibiti wa mipaka wa kielektronikia (e-Border Management)
Kabla ya kuzindua mfumo wa uhamiaji mtandao Rais Magufuli alikagua teknolojia iliyotumika katika mfumo huo ikiwa ni pamoja na kuchukuliwa alama za vidole na baadaye kupatiwa pasipoti mpya ya kielekektroniki (e-Passport) ambayo pia ilianza kutolewa Jumatano.
Rais wa Zanzibar Ali Mohammed Shein pia alipokezwa pasipoti hiyo mpya.
Dkt Magufuli aliishukuru idara hiyo kwa kuhakikisha mfumo huo wa kutoa pasipoti mpya ya kielektronikia ulifanikishwa kwa gharama ya Shilingi Bilioni 127.2 ikilinganishwa na makadirio yaliyowekwa awali ya Shilingi Bilioni 400.
"Hapa tumeokoa fedha nyingi za Watanzania, kuna watu walikuwa wamejiandaa kutupiga na kuchukua hizo Shilingi Bilioni 400, lakini tukatumia vyombo vyetu mbalimbali, tukafanya uchunguzi na tumefanikiwa kutekeleza mradi huu kwa gharama nafuu" alisema Dkt Magufuli.
Rais aliahidi kutoa Shilingi Bilioni 10 kwa ajili ya kujenga ofisi ya makao makuu ya idara hiyo mjini Dodoma.
"Kamishna Jenerali Dkt. Anna Makakala na timu yako mnafanya kazi nzuri, ndio maana nimewanunulia nyumba 103 kwa ajili ya wafanyakazi na leo nitawapa fedha nyingine Shilingi Bilioni 10 mkajenge ofisi nzuri ya makao makuu.
''Nyinyi endeleeni kuchapa kazi, endeleeni kukamata wahamiaji haramu na endeleeni kukusanya mapato vizuri," amesema Rais Magufuli.
  • Masharti ya kupata pasipoti ya kielektroniki
  • Utahitajika kuwa na Kitambulisho cha Taifa
Pasipoti hizo mpya, zitagharimu Sh 150,000 kila moja na zitatumika kwa miaka 10, kabla ya kuhuishwa tena.