Usajili wa nyota wa soka duniani akiwemo Lionel Messi, Cristiano Ronaldo, Gareth Bale na Sergio Ramos hauweza kutatua matatizo katika klabu ya Man United, kulingana na nahodha wake wa zamani Wayne Rooney.
Rooney, ambaye anaichezea klabu ya DC United nchini Marekani , hadhani kwamba kikosi cha Ole Gunnar Solskjaer kitaweza kushindana na timu nyengine msimu ujao.

''Kitu cha kwanza ambacho Ole anafaa kufanya ni kujenga kikosi hicho na sidhani kuleta mchezaji mwenye thamani £100m kutawasaidia wachezaji waliopo'' , alisema nahodha huyo wa zamani wa timu ya Uingereza, 33.
Akizungumza na BBC aliongezea, '',Ole angenunua wachezaji walio na thamani ya kati ya £30-40m wenye uwezo na baadaye kukijenga kikosi chake kutokana na wachezaji watano ama sita.
Unaweza kuwaleta wachezaji kama Messi, na mshambuliaji wa Juventus Ronaldo , Ramos na Bale lakini itakugharimu £350m na baada ya miaka miwili fedha hizo zimepotea.
Mshambuilaji wa Barcelona Lionel Messi na yule wa Juventus Ronaldo wameshinda mataji 10 ya balon D'Or huku nahodha wa Real Madrid Ramos, 33, akiwa ameshinda kombe la dunia, ubingwa wa Ulaya na mataji manne ya ligi ya mbaingwa.
Mchezaji mwenza wa Ramos, Bale, 29, ameshinda taji hilo la Ulaya mara nne na kwa kipindi kirefu amehusishwa na uhamisho wa kuelekea Old Trafford.
Rooney anataraji kwamba utakuwa wakati mgumu wa Solskjaer ambaye amehusishwa na uhamisho wa wachezaji kadhaa , ikiwemo beki wa Ajax Matthijs de Ligt.
Solskjaer, ambaye alimrithi Jose Mourinho kama mkufunzi wa United ameanza kujenga kikosi chake huku winga wa Swansea Daniel James 21 akiwa wa kwanza kuelekea Old Trafford.
Rooney ambaye amewahi kuwa mfungaji wa magoli mengi akiichezea United na Uingereza alisema: Klabu inafaa kujengwa na wachezaji wachanga lakini ni sharti wawe wazuri wa haja na nafikiri mashabiki wataelewa kwamba huenda wasipiganie taji la ligi mwaka ujao.
Wacha Ole awe na kikosi atakachokijenga kwa kipindi cha miaka miwili au mitatu ambacho kitaweza kupigania ligi ya Uingereza na ile ya mabingwa Ulaya.
Ni timu kama vile Chelsea, Arsenal na Tottenham na hususan Everton ambazo zitahitaji kipindi cha miaka miwili kufikia kiwango cha Liverpool na Manchester City.

Rooney azungumzia kuhusu England

Wayne Rooney na Gareth SouthgateHaki miliki ya pichaGETTY IMAGES
Image captionRooney alimaliza kipindi chake cha mchezo nchini Uingereza chini ya Gareth Southgate
England ililazwa 3-1 na Uholanzi katika michuano ya ligi ya kitaifa ya Ulaya siku ya Alhamisi , baada ya masikhara ya mchezaji Ross Barkley na John Stones kusababisha magoli mawili.
Rooney anaamini kushindwa huko kutaisaidia Uingereza katika siku zijazo akitumai kwamba mkufunzi Gareth Southgate ataendelea kuisaidia timu yake kucheza kutoka nyuma.
''Kila mtu alisikitishwa na hatua ya timu hiyo kushindwa kufuzu, lakini timu hiyo ina wachezaji wachanga'', alisema.
Ingekuwa bora kubeba taji hilo, lakini kulikuwa na makosa yaliofanyika uwanjani na nje na wachezaji pamoja na wakufunzi.
Southgate alitaka kuwapumzisha wachezaji sita -wachezaji watatu wa Liverpool, Jordan Henderson, Trent Alexander-Arnold , Joe Gomez, na mchezaji wa Tottenham Eric Dier, Harry Kane na Dele Alli - ambao walicheza katika ligi ya mabingwa siku tano zilizopita.
Rooney alisema: "Iwapo Gareth angekubaliwa angeliwaanzisha wachezaji walioshiriki katika michuano ya ligi ya mabingwa .
''Mimi ningewaanzisha. Walikuwa katika hali nzuri ya kimaungo na wachezaji wa Liverpool walikuwa wanatoka katika ushindi na hilo lingeweza kuleta taofauti''.
Katika makosa yaliofanyika, aliongezea ''nadhani hayo hayatafanyika tena na iwapo yatafanyika na hivyo ndivyo mkufunzi anavyotaka wacheze basi atawajibika.
''Iwapo ningekuwa katika nafasi yake ningewashinikiza kuendelea na kile wanachofanya ''.