Mjumbe mkuu wa Marekani nchini Afrika anaelekea Sudan wakati kukishuhudiwa mgogoro, idara ya mambo ya nje imesema.
Tibor Nagy, naibu waziri wa Afrika, "ataomba kusitishwa mashambulio dhidi ya raia".
Kumekuwa na mgomo wa kitaifa wa wafanyakazi, ulioanza siku ya Jumapili kuishinikiza serikali ya kijeshi kutoa fursa kuwepo kwa serikali ya kiraia.
Watu wanne wameuawa katika siku ya kwanza ya mgomo huo baada ya vikosi vya usalama kufyetua gesi ya kutoa machozi na risasi za moto.
Wizara ya mambo ya nje imesema Bwana Nagy 'ataziomba pande husika kushirikiana katika kuidhinisha mazingira' ya kuweza kuendeleza mazungumzo ya pande hizo mbili.
Ataijadili hali pia na waziri mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed, ambaye amekuwa akijaribu kuwa mpatanishi kati ya baraza la kijeshi na upinzani Sudan, kabla ya hapo baadaye kuelekea Msumbiji na Afrika kusini.
Nini kilichofanyika wakati wa maandamano?
Kulikuwa na ukimya siku ya Jumatatu mjini Khartoum, licha ya kwamba maduka kadhaa yalianza kufunguliwa na mabasi kiasi kuanza kuhudumu.
Baadhi ya maduka, soko na mabenki katika mji mkuu huo pamoja na katika miji mingine, yaliendelea kufungwa wakati wafanyakazi wakifuata maagizo ya upinzani Sudanese Professionals Association (SPA), kwamba watu wasiende kazini.
SPA uliitisha mgomo baada ya zaidi ya waandamanaji 100 wa amani kuuawa na kundi la kijeshi, Rapid Support Forces (RSF), mnamo Juni 3.
"Mgomo wa kiraia utaanza Jumapili na utamalizika wakati serikali ya kiraia itakapojitangaza katika televisheni ya taifa," SPA limesema katika taarifa yake.
"Kutotii ni hatua ya amani ilio na uwezo wa kudhalilisha silaha zenye nguvu duniani."
Waandamanaji wameweka vizuizi barabarani katika mji mkuu. Watumiaji mitandao ya kijamii waliofanikiwa kufungua intaneti wanaeleza kwamba huduma hiyo imefungwa na utawala wa kijeshi.
Katika matukio mengine, viongozi watatu wa waasi wametimuliwa kutoka mji mkuu huo na kupelekwa Sudan kusini.
Mojawapo kati ya watatu, Yasir Arman, alirudi Sudan kusini mwezi uliopita baada ya kuishi uhamishoni baada ya kuhukumiwa kifo pasi kuwepo mahakamani.
Nini kinachofuata sasa?
Jeshi lilimtimua kiongozi wa muda mrefu Omar al-Bashir mnamo Aprili baada ya maandamano ya miezi kadhaa dhidi yake. Baraza la kijeshi liliahidi kwamba utawala utakabadhiwa kwa raia.
Lakini wanaharakati wanaounga mkono demokrasia wanasema baraza la kijeshi haliwezi kuaminika baada ya msako ulioshuhudiwa Jumatatu dhidi ya waandamanaji mjini Khartoum - na wamekataa pendekezo lolote la kufanya mazungumzo.
Hatahivyo, kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, viongozi wa upinzani wameweka mipango ya serikali ya mpito itakayoongozwa na mwanauchumi maarufu nchini humo.
Wakinukuu duru kutoka muungano wa upinzani na makundi yanayoandamana, Reuters linasema upinzani utamchagua Abdullah Hamdouk, aliyekuwa katibu mtendaji wa baraza la uchumi la Umoja wa mataifa barani Afrika, kuwa waziri mkuu.
Inaarifiwa kwamba wanapanga pia kuwateua watu wanane wengine wakiwemo wanawake watatu watakaokuwepo kwenye baraza hilo la mpito.
Katika ziara yake huko Khartoum wiki iliyopita, waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed alipendekeza kitu kama hicho, kuwepo baraza la la mpito la watu 15 litakalojumuisha raia wanane na maafisa wasaba wa jeshi.
|
0 Comments