Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla akizungumza na wananchi wa Kata ya Alaitole ndani ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro alipofika kutatua mgogoro wa wananchi wa Kata hiyo kuzuiwa kujenga shule ya Wasichana ya bweni na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro katika eneo la Esere, wilayani Ngorongoro. Hata hivyo Waziri Kigwangalla ameumaliza mgogoro huo kwa kuagiza wakazi hao wapewe kibali cha ujenzi na mamlaka hiyo katika eneo lililopendekezwa. 
Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla (kushoto) akisikiliza maoni na hoja za wananchi wa Kata ya Alaitole alipofika kutatua mgogoro wa wananchi wa Kata hiyo kuzuiwa kujenga shule ya Wasichana ya bweni na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro katika eneo lao la Esere, wilayani Ngorongoro jijini Arusha. 
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia na Mbunge wa jimbo la Ngorongoro Mhe.William Ole Nasha akizungumza na wakazi wa Kata ya Alaitole iliyo ndani ya Eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ambayo ilizuiwa kujenga shule ya bweni ya wasichana na mamlaka hiyo zuio ambalo limeondolewa na Waziri wa Maliasili na Utalii aliyefika katika kata hiyo kutatua mgogoro huo. 
Mkutano wa Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla na wananchi wa Kata ya Alaitole katika Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro. Mhe. Kigwangalla alifika kutatua mgogoro uliohusisha wananchi wa Kata hiyo kuzuiwa kujenga shule ya Wasichana ya bweni na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro 
Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla akizungumza na wananchi wa Kata ya Alaitole ndani ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro mara baada ya kupitishwa na katika eneo lilipoonekana fuvu linalosadikiwa kuwa ni la binadamu wa kale ambalo bado taarifa zake zinaendelea kufanyiwa utafiti katika eneo la Esere, wilayani Ngorongoro. 
Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla akiwa ameambatana na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Ngorongoro Mhe.William Ole Nasha na askari wa uhifadhi wakiangalia eneo itakapojengwa shule ya wasichana ya bweni ya kata ya Alaitole. 
Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla, viongozi na wananchi wa Kata Alaitole wakitazama eneo lilipoonekana fuvu linalosadikiwa kuwa ni la binadamu wa kale lililogunduliwa na wakazi hao katika eneo la Esere, wilayani Ngorongoro. Taarifa kuhusu fuvu hilo zinaendelea kufanyiwa utafiti na watalaam. 
Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla akisalimiana kwa furaha na wananchi wa Kata ya Alaitole ndani ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro alipofika kutatua mgogoro wa wananchi wa Kata hiyo kuzuiwa kujenga shule ya Wasichana ya bweni na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro katika eneo la Esere, wilayani Ngorongoro. PICHA/ Wizara ya Maliasili na Utalii. 
…………………… 
WMU – Ngorongoro, ARUSHA. 
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla, ameuagiza uongozi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro uwaruhusu wananchi wa Kata ya Alaitole wajenge shule ya wasichana ya bweni katika eneo la Esere lililo ndani ya Mamlaka hiyo ili waweze kupata elimu kufuatia wananchi hao kuzuiwa kwa muda mrefu kutekeleza mradi huo. 
Aidha, ameutaka uongozi wa Mamlaka hiyo utoe kibali cha kuwawezesha wananchi kata hiyo kuanza ujenzi haraka iwezekanavyo ili fedha zilizotolewa na Serikali shilingi milioni 298 zianze kutumika. 
Dkt. Kigwangalla ametoa maagizo hayo alipokuwa akizungumza na kusikiliza kero za wananchi wa Kata Alaitole wilayani Ngorongoro kwenye mkutano wa hadhara uliowashirikisha viongozi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, viongozi serikali wa kata hiyo, viongozi wa mila wa kabila la Masai na madiwani na Mbunge wa jimbo la Ngorongoro Mhe. William Ole Nasha. 
Amesema Serikali inaunga mkono juhudi zote za wananchi za kujiletea maendeleo akifafanua kwamba hatua ya wananchi hao kuamua kujenga shule ya Sekondari ya Bweni ni jambo la linalopaswa kupongezwa na kila mpenda maendeleo. 
“Mnacho kitaka kiko wazi, mnataka maendeleo ya watoto wenu, katika hili mmesema kila baba anatoa elfu hamsini na wanawake wanatoa elfu ishirini, hili ni jambo kubwa achilia mbali nguvu kazi mnayojitolea na tayari serikali imeshaleta milioni 298, haiingii akilini eneo linalochangia kuleta na kuingiza mapato mengi Serikalini kiasi cha bilioni 126 likose shule” Amesisitiza Dkt. Kigwangalla. 
Dkt. Kigwangalla ameeleza kuwa ujenzi shule hiyo utawaondolea wanafunzi adha ya kutembea umbali mrefu akibainisha kuwa Serikali itaendelea kuwaunga mkono wananchi hao kwenye mipango yao ya utekelezaji miradi ya maendeleo. 
Amesema jamii hiyo pamoja na mazingira wanayoishi kuwa ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro wanahitaji elimu. Aidha, amesema pia ni muhimu katika sekta ya utalii kupitia utamaduni wao akiongeza kuwa kazi ya Wizara ni kuona mafanikio ya sekta ya utalii yanakuwa kwa kuongeza mapato na sio migogoro. 
Dkt. Kigwangalla amesema Hifadhi ya Ngorongoro ni hifadhi mseto inayoruhusu binadamu na wanyama kuwepo katika eneo moja na kwamba hiyo ipo kwa mujibu wa sheria akiitaka Mamlaka hiyo kuyatazama vizuri majukumu yake ya kuendeleza Utalii, Kulinda rasilimali zililizopo kwa maana ya kuhifadhi na kuhudumia jamii iliyo ndani ya hifadhi hiyo. 
Katika hatua nyingine ameutaka uongozi wa Mamlaka hiyo uendelee kufanya mazungumzo na wananchi hao badala ya kujielekeza katika matumizi ya nguvu ili kupata uelewa wa pamoja akitolea mfano wa eneo la Loliondo ambalo hivi sasa lina utulivu. 
“ Viongozi wa Mamlaka mnalo jukumu la kuwasikiliza wananchi na kuamua kwa pamoja, eneo la Ngorongoro ni Urithi wa dunia na litaendelea kuwa hivyo kwa kuheshimu na maslahi ya Taifa na maslahi ya walio walio wengi” Amesisitiza Dkt. Kigwangalla. 
Kuhusu mahusiano baina ya wananchi na wahifdhi Dkt. Kigwangalla amesema kuwa kupitia mkutano wake na wananchi amebaini kuwepo kwa tatizo la mawasiliano na mahusiano baina ya wananchi wa eneo hilo na watumishi wa Serikali walio chini ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro akibainisha kwamba tayari serikali imeliona jambo hilo na inaendelea kulifanyia kazi. 
Naye Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Ngorongoro Mhe. William Ole Nasha akizungumza wakati wa mkutano huo amempongeza na kumshukuru Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuhakikisha ulinzi wa rasilimali za Taifa katika maeneo mbalimbali nchini. 
Amemwomba aeendelee kutembelea maeneo mengine ya jimbo hilo kwa lengo la kusikiliza kero za wananchi wa kata za wilaya hiyo kwa lengo la kudumisha mahusiano mema. 
Mhe. Ole Nasha ameeleza kuwa hatua ya Wizara kutafutia ufumbuzi mgogoro huo wa ujenzi wa shule ya wasichana ya bweni, vile vile uamuzi wa serikali kutoa eneo na fedha kiasi cha shilingi milioni 298 kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo katika eneo lililokubaliwa ni ishara tosha kwamba Serikali inawalinda na kuwajali wananchi wake. 
Amesema wananchi wa jimbo la Ngorongoro pamoja na changamoto mbalimbali zinazowakabili wako ni wasikivu na wako tayari muda wote kushirikiana na Serikali ikiwemo ulinzi wa rasilimali zilizopo na kuendeleza uhifadhi katika hifadhi ya Ngorongoro. 
Kwa upande wao wananchi wa Kata ya Alaitole wakizungumza kwa nyakati tofauti wamemshukuru Dkt. Kigwangalla kwa kuamua kuwafuata na kuzungumza nao katika makazi yao wakimpongeza kwa juhudi zake za kutatua changamoto mbalimbali kwa maslahi ya wananchi na uhifadhi. 
Aidha, wamemwomba kuendelea kuisimamia sekta ya uhifadhi nchi wakitoa wito wa kudumisha mahusiano mema baina ya wananchi na wahifadhi.