WAKATI warembo 16 kutoka mkoani Manyara wakitarajiwa kupanda jukwaani Julai 19 mwaka huu siku ya Ijumaa mjini Babati kuwania taji la Miss Manyara,  msanii wa Bongo Fleva, Christian Bella, ndiye anatarajiwa kunogesha shindano hilo.

Shindano hilo litafanyika katika ukumbi wa The Champions Lounge Babati mjini ambapo  warembo 16 watapanda jukwaani kuchuana vikali kusaka taji la Miss Manyara 2019 ambaye ataenda kushindana katika mashindano ya Miss Tanzania Kanda ya Kaskazini jijini Arusha kati ya Julai 25 mwaka huu.

Mkurugenzi wa kampuni ya G.Crown Solution Agency ambayo ndiyo wandaaji wa shindano hilo, Akon Clement, amesema maandalizi yamekamilika huku akithibitisha kuwa Bella  atatumbuiza  na kiingilio ni Sh. 10,000 kawaida,  na VIP ni 20,000/=  na kuongeza kuwa shindano la mwaka huu litakuwa na changamoto kubwa kwa maana warembo wote wameonyesha uwezo wa hali ya juu.
Christian Bella.
Amesema awali walijitokeza warembo 21 kushiriki mashindano hayo kabla ya mchujo kufanyika na kupatikana warembo 16 ambapo walitumia kigezo cha umri, mvuto, uwezo wa kujitambua na kujieleza  na mengine mengi.
Akon amesema warembo hao wakiwa kambini waliweza kutafutiwa wataalam wa fani na taaluma mbalimbali ambao walikuwa wanawafundisha kuhusiana na stadi za maisha kwani wanaamini kwa kupitia warembo hao mkoa wa Manyara utatangazika vyema.
Alisema shindano litaanza majira ya saa moja na nusu za usiku na kuongeza kuwa wapo wadhamini waliojitokeza kuwapa sapoti baada ya kushindwa kufanya shindano hilo kwa miaka miwili mfululizo kwa kuhakikisha mwaka huu kila kitu kinaenda sawa ambao ni Mati Super Brand Limited kama mdhamini mkuu huku wengine wakiwa ni Tarangire National parks, Asmirein Hotel, Bonite Bottlers Limited kupitia kinywaji chao cha Coca Cola na Hamadi Kubeti.
Kwa upande wa zawadi,  alisema zimeboreshwa, tofauti na miaka ya nyumba, ambapo mwaka huu mshindi wa kwanza atapata shilingi milioni moja na nusu, wa pili milioni moja, mshindi wa tatu ataondoka na laki tano huku nafasi ya nne hadi 16 watapata shilingi laki mojamoja kama kifuta jasho.
Habari na Kennedy Lucas, Manyara.