DAR ES SALAAM: Hii ni rekodi ya kibabe! Mrembo anayefanya vizuri mno kwenye anga la Bongo Fleva, Faustina Charles Mfinanga ‘Nandy’ (26), ameonesha kwamba ukiamua kuweka ndoto zako na kusaka namna ya kuzitimiza, hakika inawezekana, Ijumaa linaripoti!
Nandy au The African Princess ameweka rekodi ya kibabe kwa kumiliki magari mengi ya kifahari akiwa angali na umri mdogo wa miaka 26 tu huku akiwa na muda mchache kwenye gemu la Bongo Fleva, miaka mitatu na ushee hivi!
NDINGA MPYA
Mapema wiki hii, mrembo huyo ameshtua ulimwengu wa burudani Bongo kwa kuonesha mkoko wake mpya wa kifahari aina ya Land Rover Discover TDV6 HSE.
IDADI YA JUMLA
Ndinga hilo jipya alilolinunua hivi karibuni, linaongeza idadi ya magari anayomiliki mrembo huyo ambayo ameyanunua kwa nyakati tofauti hadi kufikia sita. Katika magari hayo sita, yapo ambayo gharama zake zinacheza kwenye zaidi ya shilingi milioni 30, lakini pia yapo ya chini ya hapo.
MAGARI YENYEWE
Ukiachana na Land Rover Discover TDV6 HSE, mrembo huyo anayesumbua na Wimbo wa Hazipo, katika orodha yake hiyo ya magari, limo BMW X1, Mercedes Benz E-Class E320 CDI, Toyota Alphard, Toyota Harrier na Toyota Noah ambayo anayatumia kwa shughuli zake mbalimbali.
ANAYATUMIAJE?
Kwa mujibu wa mtu wa karibu wa mwanamuziki huyo, magari hayo anayatumia kwa shughuli zake mbalimbali ikiwemo muziki pamoja na bidhaa nyingine za urembo kwani anasambaza pia bidhaa za urembo zenye jina lake.
“Yapo haya magari ya kifahari kama Land Rover Discover, BMW na Benz mara nyingi anayatumia kwa kutembelea yeye mwenyewe anapokuwa kwenye shughuli zake binafsi. Mathalan akiwa anakwenda klabu kwenye shoo au anataka kwenda mkoa wa jirani kwa kutumia usafiri wa ardhini, basi huchagua gari analoona linafaa kwa safari yake kwa kuzingatia usalama wake,” alilieleza Ijumaa mtu huyo ambaye hakupenda jina lake lipambe ukurasa huu.
ATANGAZWA KUWA BOSS LADY
Baada ya tu ya kuonesha ndinga lake hilo jipya, kurasa mbalimbali za wachambuzi wa burudani kwenye Instagram zimemtangaza rasmi Nandy kuwa Boss Lady kutokana na kumiliki idadi hiyo ya magari ambayo kimsingi inaaminika kwamba huwezi kuwa nayo kama akaunti yako benki inasoma chini ya shilingi milioni 50 na huna miradi zaidi ya mmoja ya kukuingizia fedha.
“Nandy kwa sasa anastahili kuwa Boss Lady kama walivyo akina Zari (Zarinah Hassan) na wengineo ambao tunawaona wanatembelea magari ya kifahari na wanaishi pazuri,” moja ya kurasa maarufu za Instagram ulichagiza.
AWAFUNIKA LYNN, LULU DIVA
Nandy anaweka rekodi ya aina yake kwa warembo wanaofanya muziki wa Bongo Fleva kwa uwezo wa kimuziki pamoja na kumiliki magari ya kifahari.
MAGARI YA LYNN
Anamuacha mbali Irene Hillary ‘Lynn’ ambaye rekodi zinaonesha ana magari manne ya kifahari ambayo ni BMW Z3, Volkswagen Touareg, Toyota Mark X na Jaguar X-Type.
LULU DIVA JE?
Kwa upande wake, Lulu Abbas ‘Lulu Diva’, yeye anatikisa zaidi na mkoko mmoja wa maana aina ya Jeep ‘Liberty’, toleo la nchini Marekani.
MAFANIKIO YA NANDY
Akizungumza na Ijumaa, mrembo huyo ameweka wazi siri ya mafanikio yake kuwa ni kujituma na kujiwekea malengo katika kazi zake.
“Siri ya mafanikio yangu inatokana na juhudi zangu. Pia nina menejimenti nzuri ambayo ipo siriazi sana linapokuja suala la kazi, ndiyo maana imenifanya niwe na mafanikio haya na hivi karibuni natarajia kufungua kampuni yangu nyingine ila siwezi kusema ni ya nini kwa sababu kuna mambo ambayo bado tunayaweka sawa, yakikamilika, basi kila mtu atajua,” alisema Nandy.
Licha ya Nandy kutoanika miradi yake mingine, lakini Gazeti la Ijumaa linafahamu ana kampuni ya bidhaa za urembo na pia ni balozi wa kinywaji kikubwa Afrika Mashariki. Nandy pia siku za hivi karibuni amekuwa akiweka rekodi ya kujaza watu wengi kwenye shoo za uwanjani. Kama unakumbuka, miongoni mwa balaa alilolifanya ni shoo ya kuujaza uwanja wa Nelson Mandela, Sumbawanga katika Sherehe ya Idd Mosi.
0 Comments