LEO ni siku ya siku 62 yaani miezi miwili tangu Klabu ya Yanga ilipofanikiwa kuwapata viongozi wake wapya katika uchaguzi mkuu uliofanyika Mei 5, mwaka huu. Tangu viongozi wapya walioingia madarakani wakiongozwa na mwenyekiti, Mshindo Msolla na makamu wake, Fredrick Mwakalebela, uongozi huo umefanikiwa kufanya mambo makubwa ndani ya muda mfupi.
Ndani ya muda huo, wamefanikiwa kuboresha baadhi ya vitu ndani ya klabu hiyo kuhakikisha wanatekeleza yale ambayo waliyaahidi kwa wapiga kura ambao ndiyo waliosababisha hivi sasa wameingia madarakani. Gazeti la Championi Ijumaa linakuchambulia baadhi ya vitu ambavyo viongozi hao wameonekana kuvifanyia kazi kwa muda mfupi na kuleta matumaini mapya.
KUBWA KULIKO
Viongozi hao kwa kushirikiana na Kamati ya Hamasa chini ya mwenyekiti wake, Antony Mavunde, wameshirikiana vyema kufanikisha Tamasha la Kubwa Kuliko lililofanyika Juni 15 na kufanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi milioni 930. Jambo hili limefungua mwanga mpya ndani ya klabu hiyo kwa kuondokana na utegemezi huku ikiwafungua wadau mbalimbali kuweza kujitolea katika timu yao.
Ikumbukwe kuwa tangu kuondoka kwa Yusuf Manji ambaye alikuwa mwenyekiti wa klabu hiyo, ni kama mambo yalibadilika na ukata ukatawala klabuni hapo.
USAJILI WA WACHEZAJI
Kwa asilimia kubwa viongozi hawa wamefanikiwa kufanya usajili wa wachezaji ndani ya Yanga kwa asilimia 90 na Msolla amesema katika usajili huo umezingatia kila alichokuwa akihitaji kocha mkuu wa timu hiyo, Mwinyi Zahera.
Hiyo inaonyesha ni mafanikio mkubwa ambayo wameyapata chini ya uongozi huo mpya baada ya msimu uliopita kusajili kwa kusuasua.
Baadhi ya wachezaji wa kimataifa waliosajiliwa ni Farouk Shikhalo raia wa Kenya, Mustafa Suleiman (Burundi), Lamine Moro (Mghana), Patrick Sibomana (Rwanda), Juma Balinya (Uganda) Maybin Kalengo (Zambia), Issa Bigirimana (Rwanda) na Sadney Urikhob (Namibia), huku wazawa wakiwa Ally Mtoni, Ally Ally, Abdulaziz Makame na Mapinduzi Balama.
SIKU YA MWANANCHI
Klabu ya Yanga kwa sasa imeanzisha Siku ya Mwananchi ambayo itahusisha kufanya mambo mbalimbali ya kijamii kama ilivyo kwa Klabu ya Simba ambayo huwa na Simba Day.
Maadhimisho ya Siku ya Mwananchi yataanza Julai 21 hadi 27 ambapo ndiyo itakuwa hitimisho kwa kucheza mechi moja ya kimataifa ya kirafiki pamoja na kuwatambulisha wachezaji wapya na jezi mpya za msimu ujao jambo ambalo halikuwepo huko nyuma.
MABADILIKO YA MFUMO WA UONGOZI
Viongozi hao wapya ndani ya Yanga wameamua kuja na mkakati mpya ndani ya klabu hiyo katika mfumo mzima wa uongozi ambao wameufanyia mabadiliko ambayo huko nyuma hayakuwepo.
Klabu ya Yanga hivi sasa itakuwa na mtendaji mkuu ambaye atasimamia masuala yote ya utendaji wa klabu kwa
kuwasimamia wakurugenzi ambao wataajiriwa ikiwa ni mfumo mpya. Hapo kabla haukuwepo. Pia kamati ya utendaji itakuwa ikifanya kazi bila ya kuingiliana.
kuwasimamia wakurugenzi ambao wataajiriwa ikiwa ni mfumo mpya. Hapo kabla haukuwepo. Pia kamati ya utendaji itakuwa ikifanya kazi bila ya kuingiliana.
KUFANYA VITU KWA UWAZI
Uongozi huu wa sasa umeweka mkakati wa kufanya mambo yake yote kwa uwazi hasa katika suala zima la fedha ambapo wamedhamiria kuhakikisha kila fedha inayoingia klabuni hapo inakuwa wazi kwa lengo la kudhibiti uchakachuaji.
KUDHIBITI VYANZO VYA MAPATO
Hivi karibuni uongozi huo ulitangaza mkakati wake wa kudhibiti watumiaji holela wa nembo ya klabu ambapo wamepanga kukutana nao ikiwa ni sehemu ya kudhibiti mapato ya klabu hiyo kongwe.
Huu ni mwanzo mzuri, kama haitakuwa nguvu ya soda inamaanisha kuwa Yanga ya sasa inaweza kuwa na mwendelezo mzuri, mashabiki wa timu hiyo wamerejeshewa furaha.
Na sasa ule ushindani mkali kati ya Simba na Yanga utakuwa na nguvu kubwa baada ya awali kuonekana ni Simba pekee ndiyo wana nguvu kubwa kutokana na kuwa vizuri kiuchumi. Inavyoonekana mikakati yao inafanikiwa kwa asilimia 80 na kilichobaki ni asilimia 20 ambazo zitaonekana uwanjani kwa timu itakapoanza kazi.
0 Comments