Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta hii leo{jana} anafanya ziara binafsi ya siku mbili nchini Tanzania ambapo anapokewa na mwenyeji wake rais John Magufuli wa Tanzania.
Taarifa rasmi kutoka Ikulu ya Tanzania imeeleza kuwa marais hao wawili wa mataifa jirani watakutana kijijini kwa Magufuli wilayani Chato.
Mkutano huo unakuja katika kipindi ambacho uhusiano wa nchi hizo mbili unamulikwa na kurunzi.
Rais Uhuru Kenyatta aliwasili jioni hii huko Nyamirezi katika uwanja wa ndege wa Chato katika mkoa wa Geita.
Katika mapokezi yake, Rais Uhuru Kenyatta alieleza furaha yake kujumuika na Watanzania na kumshukuru rais Magufuli kwa mualiko wake.
Amesema dhamira ya ziara hiyo ni kuimarisha uhusiano wa kijirani baina ya kenya na Tanzania.
Ameeleza umuhimu wa viongozi kuwajibika kuhakikisha kuondosha vikwazo vinavyozuia kufanya biashara, kuruhusu mzunguko huru wa watu na kuzidi kuimarisha uhusiano na kusisitiza umuhimu wa mataifa ya Afrika mashariki kushikana kama kitu kimoja.
Kwa upande wake, mwenyeji rais John Magufuli amesisistiza lengo la taifa lake kuendelea kutunza uhusiano wa kieneo.
'Tuendelee kushikamana na kuwa kitu kimoja, tusikubali kulaghaiwa' amesema kiongozi huyo wa Tanzania.
Faida ya pamoja Afrika mashariki:
Katika hotuba yake alipowasili Uhuru Kenyatta, alisisitiza kuhusu mshikamano wa kieneo na kueleza kuwa taifa moja linaponufaika ni faida kwa taifa jirani.
Katika kuonekana kugusia mzozo wa hivi karibuni uliotokana na kauli aliyotoa mbunge wa Kenya, Jaguar, Charles Njagua Kanyi, maarufu Jaguar, ilioibua hisia kali kieneo, Rais Uhuru ameeleza:
'Wanasiasa shida yao wengine wanaongea bila ya kufikiria, mtu anajiona pahali ameishi, anafikiria hapo ndipo mwisho wa dunia. Wengine wanaropoka mambo ambayo hayapo'.
'Wawezaje kumwambia Mtanzania huwezi kufanya biashara Kenya? Wawezaje kumwambia Mtanzania huwezi kutembea Kenya? Wawezaje kumwambia Mtanzania hawezi kutafuta bibi Kenya? vile vile huwezi kumzuia Mkenya aje Tanzania kufanya biashara yake...huwezi kumzuia Mkenya akiwa ameona mtoto hapa Chatu aje hapa amnong'onezee kidogoo.. na hiyo ndio East Afrika tunayoitaka' ameongeza rais Uhuru Kenyatta akihotubia umati wa watu waliokusanyika katika uwanja wa ndege huo wa Chatu huko Geita.
Mbunge huyo alikamatwa kwa matamshi ya uchochezi dhidi ya raia wa kigeni ambayo hayakuchukuliwa kirahisi na bunge la Tanzania, ameshapandishwa kizimbani na yupo nje kwa dhamana.
Matamshi ya Jaguar yamesababisha vita vya maneno na kuongeza chumvi kwenye kidonda.
Matukio manane yaliotia mashakani uhusiano baina ya Kenya na Tanzania
Mwezi Julai mwaka 2017 Mataifa ya Tanzania na Kenya yalifanikiwa kuandaa mkutano ambao ulilenga kuondolewa kwa marufuku ya bidhaa zinazoingia katika mataifa hayo mawili kutoka pande zote mbili.
Aliyekuwa Waziri wa maswala ya kigeni na ushirikiano wa Afrika Mashariki wakati huo Dkt. Augustine Mahiga alitangaza uamuzi huo jijini Nairobi kufuatia majadiliano kati ya rais John Pombe Magufuli wa Tanzania na Uhuru Kenyatta wa Kenya.
Na kufuatia hatua hiyo Kenya iliondoa marufuku ya Unga wa ngano na Gesi inayoingia nchini humo kutoka Tanzania huku Tanzania nayo ikiondoa marufuku ya sigara na maziwa kutoka Kenya.
Kuongezea, mataifa hayo mawili yaliahidi kuanzisha kamati ya pamoja kuangazia maswala tofauti.
Uhusiano wa kidiplomasia na kibiashara kati ya Kenya na Tanzania uliathiriwa kwa muda huku mataifa yote mawili yakiweka marufuku hizo.
Marufuku ya bidhaa kutoka Tanzania kuingia Kenya ilitokana na wasiwasi wa kiusalama na ubora wa bidhaa huku Tanzania ikijibu kwa kuweka marufuku kwa bidhaa za Kenya kama vile matairi ya gari, mafuta ya kupaka mkate na maziwa.
Tanzania pia ilipiga marufuku usafirishaji wa mahindi kutoka Zambia kuelekea Kenya, ambayo inakabiliwa na wakati mgumu wa ukosefu wa zao hilo muhimu.
Marufuku hizo, ikilingamishwa na idadi kubwa ya bidhaa zinazotoka na kuingia katika nchi hizo zinaweza kuathiri pakubwa biashara.
Rais Uhuru Kenyatta anatarajiwa kukamilisha ziara yake siku ya Jumamosi Tanzania.
|
0 Comments