Takriban watu saba wameuawa katika shambulio moja la hoteli kusini mwa Somalkia ikiwemo mwandishi wa runinga mwenye uraia wa Canada na Somali Hodan Nalayeh, kulingana na ripoti.
Maafisa na wale walionusurika wanasema kuwa mlipuaji wa kujitolea muhanga aligongesha gari lililojaa vilipuzi katika Hoteli ya Asasey katika bandari ya Kismayo kabla ya washambuliaji hao kuvamia jengo hilo.
Nalayeh na mumewe wameripotiwa kuwa miongoni mwa wale waliouawa.
Kundi la wapinganaji la al-Shabab limekiri kutekeleza shambulio hilo.
Walioshuhudia wanasema kuwa walisikia milio ya risasi baada ya bomu lililokuwa ndani ya gari hilo kulipuka.
Haijulikana iwapo washambuliaji hao walisalia ndani ya hoteli hiyo baada ya mlipuko huo.
Afisa wa usalama Abdi Dhuhul aliambia chombo cha habatri cha AFP kwamba waziri mmoja wa utawala wa eneo hilo pamoja na wakili ni miongoni mwa waliofariki.
Vyombo vya habari katika eneo hilo na muungano wa waandishi wa Somali unasema kuwa Nalayeh ,43, pamoja na mumewe ni miongoni mwa wale waliouawa.
Runinga ya Integration TV - inayoonyesha kipindi cha lugha ya kiingereza kilichoandaliwa na kutangazwa na Nalayeh - kiliambia BBC hakijathibitisha habari hizo.
Nalayeh alitumia runinga hiyo kuelezea hadithi kuhusu maisha nchini Somalia na ughaibuni .
Vipindi vya hivi karibuni vilikuwa vikiangazia wafanyibiashara wanawake nchini Somalia na vitu vya kufanya katika mji wa Las Anod.
Alihamia nchini Canada na familia yake alipokuwa na umri wa miaka sita kabla ya kuwa mtu maarufu wa jamii ya Somalia nchini humo.
Lakini mama huyo wa watoto wawili alikua amerudi nchini Somalia hivi karibuni.
Mwandishi wa BBC Farhan Jimale alimtaja kuwa mtu mwenye 'nafsi nzuri'.
Muungano huo wa waandishi unasema kuwa Nalayeh na ripota mwengine kwa jina Mohamed Omar Sahal walikuwa watu wa kwanza kuuawa nchini humo mwaka huu.
Kundi la wapiganaji wa al-Shabab lilifurushwa mjini Kismayo 2012 na bandari hiyo imekuwa na amani katika miaka ya hivi karibuni ikilinganishwa na maeneo mengine ya kusini na katikati ya Somalia.
Wapiganaji hao wamekuwa wakitekeleza mashambulio ya mara kwa mara katika mji mkuu wa Mogadishu , licha ya kuwepo kwa idadi kuu ya wanajeshi wa Umoja wa Afrika pamoja na wale wa Somalia waliofunzwa Marekani.
0 Comments