Justin Shonga
UPO uwezekano wa mshambuliaji Mganda, Emmanuel Okwi kurejea Simba baada ya dili lake na Klabu ya Fujairah ya Falme za Kiarabu kugonga mwamba huku Simba nao wakigonga mwamba katika jitihada za kumsajili Mzambia, Justin Shonga kutoka Orlando Pirates.


Inaelezwa kuwa  wamepata straika mwingine, hivyo kuachana na mpango wa kukamilisha usajili wa Okwi, hatua ambayo imesababisha Mganda huyo aanze kusikilizia nafasi ya kurejea ‘nyumbani’ Msimbazi.

Simba ilikuwa inasaka straika wa kuziba nafasi ya Okwi, na chaguo la kwanza lilikuwa kwa Walter Bwalya raia wa Zambia anayeichezea Nkana lakini wanaelekea kushindwana dau baada ya klabu yake kusisitiza inataka Sh milioni 800.

Simba iligeuzia ndoano zake kwa Mzambia mwingine, Shonga kutoka Orlando Pirates ya Afrika Kusini, lakini “wamekatwa maini” baada ya kuambiwa kwamba Al Ahly wamepeleka ofa ya dola milioni 1 (zaidi ya Sh bilioni 2) ambazo hawawezi hata kufikiria kutoa nusu yake.

Shonga, 22, alimaliza akiwa mfungaji bora namba mbili wa Pirates msimu uliopita na amezivutia klabu nyingi Afrika.
Kwa mujibu wa magazeti ya Misri, SuperKora na Youm7, Al Ahly ipo tayari kutoa dola milioni moja inayotakiwa na Pirates, na ipo tayari kumpa mkataba wa miaka mitatu. Shonga amefunga mabao 16 na kutoa asisti 16 pia katika mechi 66 tangu atue klabuni hapo.

Simba wamekuwa wagumu kuelezea kuhusiana na sakata hilo na sasa wapo kambini Afrika Kusini wakiendelea kujifua.