Ujumbe wa Tanzania uliojumuisha wafanyabiashara kutoka sekta binafsi na baadhi ya wakuu wa mashirika ya umma (pichani) wamefanya ziara ya kibiashara nchini Brazil yenye lengo la kutafuta fursa  za kibiashara, uwekezaji na masoko  kwa bidhaa zinozalishwa Tanzania.Ziara hii ilianza tarehe 28 Juni ina itakwenda hadi 08 Julai, 2019.


Ziara hiyo  ya siku kumi imebuniwa na sekta binafsi  kwa mashirikiano na ubalozi wa Brazil nchini Tanzania na kuratibiwa kwa pamoja na Wizara ya Mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika mashariki na Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Brasilia, imejumuisha washiriki kumi na mbili ( 12) kutoka wizara ya mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika mashariki, ofisi ya ubalozi wa heshima wa Brazil nchiniTanzania, jumuiya ya wafanya biashara Tanzania; kampuni ya Zest limited na Kampuni ya Alpha Group Afrika.  Washiriki wengine katika ziara hiyo ni kampuni ya  KC Land Development Plan, Kampuni ya Pivotec Company Ltd pamoja na Shirika la biashara la Taifa la Zanzibar(ZSTC), Mamlaka ya Uthibiti wa Matumizi wa Maji na Nishati Zanzibar(ZURA) na LAM Consultant. 

Katika Ziara hiyo ujumbe wa Tanzania umeonana na kufanya mazungumzo na Taasisi mbali mbali za Brazil zikiwemo  shirika kuu la uchimbaji mafuta  na gesi la Brazil (Petrobras), kampuni ya shughuli za idhibiti wa viwango na uendelezaji  wa masoko ya mafuta na gesi (IBP), Wakala wa uwekezaji na Biashara  ya Brazil (APEX), Muungano wa Jumuiya ya Wenye viwanda ya Brazil(NCI) na Taasisi ya Uendelezaji wa Wazalishaji wadogo na Wakati (SEBRAE).  Taasisi nyingine ambazo ujumbe huu ulikutana na viongozi na kuwa na mazungumzo ya ushirikiano ni Bodi ya Utalii ya Brazil(Embratur), Wizara ya Kilimo, Sehemu ya udhibiti wa biashara za Mazao ya matunda na mifungo, Muungano wa Wenye viwanda wa São Paulo na Taasisi ya uendelezaji wa Teknolojia na ubunifu (São Paulo Technlogy Incubator) ya mjini São Paulo.


Hali kadhalika, ujumbe wa Tanzania ulipata nafasi ya kutembelea Miji mbali mbali ya Brazil ikiwemo Rio de Janeiro , Brasilia, na São Paulo pamoja na kufanya mazungumzo  na Kaimu Balozi na Maofisa wa Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Brasilia na kukutana na Jumuiya ya Watanzania (Diaspora)  waishio mjini São Paulo.


Katika mazungumzo na shirika la uchimbaji wa mafuta na gesi la Petrobras na Kampuni ya uendelezaji wa masoko na Udhibiti wa mafuta na gesi (IBP) ilibainika kwamba pamoja na kampuni ya Petobras kusitisha shughuli zake za utafutaji wa mafuta nchini Tanzania, nchi hizi mbili zinaweza kuendeleza kushirikiana katika maeneo mbalimbali yakiwepo kujenga Uwezo, kuendeleza utafiti, kukuza masoko na shughuli za udhibiti wa bidhaa na viwango katika sekta ya mafuta na gesi, pamoja na kubadilishana uzoefu na wataalamu. Ili kuhakikisha utekelezaji wa maazimio yaliyokubaliwa pande mbili ( IBP na Jumuiya ya Watoa Huduma ya Mafuta na Gesi Tanzania-ATOGS ) zimekubaliana kuandaa mkataba wa ushirikiano na kusainiwa mara baada ya kukamilisha taratibu zinazohitajika.

Kuhusu masuala ya biashara na uwekezaji imeonekana kwamba kuna uwezekano mkubwa kwa bidhaa za Tanzania kama vile korosho, karafuu na mazao ya bahari kupata soko nchini Brazil. Pia wajumbe wamebaini kuwa kuna uwezekano mkubwa kwa Tanzania kununua sukari kutoka Brazil. Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Brasilia umeahidi kufuatilia upatikanaji wa masoko hayo. Brazil ni mzalishaji mkubwa wa sukari na mazao ya mifugo.


Katika mazungumzo yaliyohusu ushirikiano wa uwekezaji kati ya nchi mbili yaliyofanyika katika Makao makuu ya wakala wa uwekezaji wa Brazil (APEX) mjini Brasília ilibainika kuwa Tanzania ina nafasi kubwa ya kujifunza katika taratibu za kuvutia wawekezaji kutoka nje na kuendeleza wawekezaji wa ndani. Pia pande mbili zilikubaliana kushirikiana katika kuendeleza fursa za uwekezaji na kubadilishana Taarifa. Vile vilewajumbe walikubaliana kuhusu umuhimu wa kuwa na taarifa za kutosha kuhusu fursa za uwekezaji zilizopo Tanzania, hivyo wito ulitolewa kwa ofisi za Ubalozi wa Tanzania Brasilia, Ubalozi wa Brazil nchini Tanzania, wakala wa uwekezaji wa Brazil , mamlaka za uwekezaji Tanzania na jumuiya ya wafanya biashara na sekta binafsi Tanzania kuimarisha ushirikiano wa karibu sana kwa lengo la kuimarisha uwekezaji na kukuza biasharakwa maslahi ya maendeleo ya uchumi wa nchini hizi mbili.  



Kutokana na ziara hii, ujumbe wa Tanzania pia ulipata nafasi ya kuzungumza na viongozi wa Taasisi inayohusika na kuendeleza wazalishaji wadogo wadogo na wa kati (SEBRAE) nchini Brazil. Mazungumzo hayo yalifanyika katika makao makuu ya ofisi hiyo yaliyopo mjini Brasilia. Baada ya mazungumzo hayo pande mbili zimekubaliana kuimarisha ushirikiano katika maeneo ya kubadilishana wataalam, uzoefu, na kujenga uwezo hasa kutokana na nchi ya Brasil kupiga hatua kubwa na kufanikiwa kuleta maendeleo katika kuimarisha uwezo wa wazalishaji wadogo wadogo na wa kati hasa wanawake. Pia ujumbe wa Tanzania ulitoa mwaliko kwa Viongozi wa taasisi hiyo na baadhi ya wazalishaji wa Brazil kutembelea Tanzania mwezi wa Oktoba wakati wa Tanzania Expo.



Kuhusu mazungumzo yaliyofanyika kati ya ujumbe wa Tanzania na Jumuiya ya Muungano wa viwanda wa Brazil, pande mbili zimekubaliana kwamba nchi hizi mbili zinashabihiana kimazingira, kijiografia, mila na utamaduni. Hivyo kuna haja kubwa wa kuimarisha mahusiano, kubadilishana wataalam, habari, na kukuza technologia ya uzalishaji katika viwanda. Brazil imeonesha nia ya kusaidia Tanzania katika kujenga uwezo wa wataaman wake kwa kutumia taasisi zake za mafunzo ya Technologia na kuendelea uzalishaji katika sekta ya viwanda. Kwahivyo imeonekana kwamba kuna haja ya kuweka saini makubaliano ya ushirikiano wan chi hivi mbili kati ya Jumuiya ya Muungano wa Viwanda wa Brazil na Jumuiya ya sekta binafsi pamoja na Jumuiya ya wafanyabiashara, wenye viwanda na wakulima wa Tanzania. Hatua hiyo itafikiwa baada ya kukamilisha taratibu za mikataba ya kimataifa



Kwa upande wa utalii imebainika kwamba licha ya kuwa Brazil na Tanzania kuwa zina mazingira na vivutio vinavyolingana vya utalii, Brazil inapokea zaidi ya mara tatu ya idadi ya watalii wanaotembelea Tanzania. Hivyo Tanzania ina mengi ya kujifunza kutoka kwa ndugu zao wa Brazil. Wito umetolewa kwa pande mbili kushirikiana kwa kubadilishana uzoefu, taarifa na utalamu pamoja na kutembeleana.