Kauli ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo nchini Tanzania, Dk. Harrison Mwakyembe ya kusema kwamba kuanzia tarehe 28 Agosti 2019 ndio itakuwa mwisho wa kutumia kazi za wasanii nchini humo bila kulipia, imezua utata mtandaoni na huku watu wakihoji kama utatekelezeka.

"Ni mwisho wa kazi ya sanaa kutumika bila kulipwa, kwenye kumbi zote za starehe iwe harusi au kitchen party watachangia, Inakuwaje Mshehereshaji (MC) anapiga muziki katika sherehe bila kulipia muziki anaotumia wakati yeye analipwa.
Ukiwa hotelini au kwenye daladala/Basi yenye mfumo wa burudani ya muziki au filamu lazima hiyo burudani iwe imelipiwa, kila mtu anapaswa kulipia" waziri Mwakyembe alisisitiza.
Waziri huyo aliongeza kuwa jambo hilo la kulipia sanaa sio jipya kwani duniani kote wasanii wanalipwa kwa kazi zao.
"Nchi zilizoendelea walianza zamani kuwalipa wasanii wao na sasa ili tuendelee lazima tulipe".
"Tanzania tulichelewa sana kukubali kuwa sanaa ni kazi , kwa sababu utamaduni wetu kwa muda mrefu kuona sanaa sio biashara bali ni urithi wa jamii fulani, burudani isiyo rasmi na historia ya ujamaa ilichangia sana".
Na katika kufanikisha hilo serikali imeamua kufanya jitihada ya kukaa na wasanii ili kuwashirikisha na kutaka kujua ni nini ambacho wanakitaka kwa sababu, imeeleza kwamba 'haiwezekani msanii anayetengeneza wimbo wake lakini lazima msanii huyo ndio alipe ili wimbo wake uweze kupigwa kwenye redio'.
Serikali ya Tanzania inataka sanaa ibadilike na imatoa wito wa ushirikiano kutoka kwa kila mmoja.
"Tukiyumba katika hili kwa kuweka umimi, siasa za tukose sote, ujuaji na ubishi usio na tija basi mafanikio hatuwezi yafikia" amesema Mwakyembe
Waziri huyo alieleza kuwa ni wakati muafaka wa sanaa kuonekana kuwa ni kazi kama kazi nyingine hivyo inapaswa kuheshimiwa.
"Lazima vyombo vyote kuongea lugha moja ili kulinda maslahi ya wanamuziki,
Tutaondoa migongano ya kisheria katika usimamizi wa sanaa nchini Tanzania".
Baadhi ya wasanii wamepokea vyema mfumo huu wa mrabaha na kusema kwamba ni jambo ambalo lilipaswa kuanza muda mrefu.
Lakini pia wasanii wanapaswa kuwa na uelewa pale ambapo redio au wanaolipia watapaswa kuchagua nyimbo gani wazilipie licha ya kuwa ni changamoto kwa wasanii wanaoanza lakini cha muhimu ni kufanya kazi kwa bidii.
"Tatizo kubwa tulilonalo duniani ni usawa, wewe unayeanza sasa hivi ni kweli watapata kidogo tofauti na wa sasa, haki iwe moja lakini hatuwezi kuwa sawa", Elizabeth Michael msanii wa filamu za Tanzania.

Kenya wasanii wanalalamikia malipo duni

Wanamuziki wa kundi la Elani wanadai kushangazwa na malipo ya chini waliyopewa na Taasisi ya haki miliki ya muziki nchini KenyaHaki miliki ya pichaELANIMUZIKI/FACEBOOK
Image captionWanamuziki wa kundi la Elani wanadai kushangazwa na malipo ya chini waliyopewa na Taasisi ya haki miliki ya muziki nchini Kenya
Taasisi ya haki miliki ya muziki nchini Kenya inakabiliwa na shutuma kali kutoka kwa wasanii wa muziki wanaodai limekuwa haliwalipi pesa zao kulingana na kazi yao.
Taasisi hiyo -Music Copyright Society of Kenya ina jukumu la kuwalipa wasanii wa muziki kwa kazi yao, lakini kwa miaka wasanii wa Kenya wamekuwa wakilalamika kuwa haliwalipi ili hali miziki yao inachezwa kwenye redio na televisheni.
Tulipe Pesa zetu, Tafadhali. Yamekuwa ni maneno yanayorudia mara kwa mara kila mara wanamuziki wanapokutana kwa mikutano yao na katika maandamano ya mitaani yanayolenga kupinga kutolipwa na taasisi hiyo. Hata hivyo bado hawajawahi kusikilizwa.
Kutokana na video yao kwenye mtandao wa Youtube wakielezea masaibu yao, Wakenya alianzisha malalamiko yao kwenye mitandao ya haabari ya kijamii kupitia kampeni iliyoitwa #ElaniSpeaks ....Ikimaanisha #ElaniWaongea:
Kuongea kwa Elani, kuliibua gumzo, huku wasanii wengine wakichochewa kufichua kiwango kidogo cha pesa ambazo walilipwa awali kwa nyimbo ambazo zilikuwa maarufu nchini .
Msanii Gidi Gidi alituma ujumbe wake wa Twitter uliosema: "Nyinyi watu mna bahati mlilipwa Shilingi 31,000; nyakati zetu tulipata Shilingi 5,000 baada ya miaka miwili ya kibao Unbwogable".