Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli amesema kuwa anatamani msanii wa muziki ,Rajab Abdul maarufu kama Harmonize au 'konde boy' kugombea nafasi ya ubunge katika jimbo la Tandahimba mkoani Mtwara, limeripoti gazeti la Mwananchi nchini Tanzania.
Rais Magufuli amesema hayo katika mkutano wa hadhara , mara baada ya msanii huyo kutumbuiza katika mkutano huo huko mkoani Lindi.

Harmonise amekuwa akikaribishwa kutumbuiza katika mikutano mbalimbali ya hadhara inayofanya rais Magufuli mara baada ya kutoa wimbo wake wa Magufuli.
Wimbo huo wa Magufuli ulioimbwa kwa mdundo wa nyimbo yake ya zamani ya kwangaru, umemsifu Magufuli kwa kazi aliyoifanya katika taifa hilo.
"I wish ningemuona Magufuli nimpigie magoti na kumpongeza hadharani...mchapakazi hachoki...Fly over sasa tunazo, Airport imeshajengwa...acha nikupongeze kwa Air Tanzania..."wimbo wa Harmonise unaoitwa Magufuli.
Lakini swali ni je, mwanamuziki huyo ataonesha nia kwa uchaguzi ujao ambao maandalizi ya uchaguzi tayari yameanza?
Iwapo Harmonise atagombea wadhfa huo wa ubunge basi anaweza kuwa msanii wa kwanza maarufu kuchukua kiti cha ubunge kupitia chama tawala.
Presentational grey line
Presentational grey line
Kwa Afrika mashariki , mwanamuziki kuwa kiongozi sio jambo geni. Tayari taifa hilo limekuwa na viongozi ambao ni wabunge ingawa wote wanatokea chama cha upinzani.
Prof.JayHaki miliki ya pichaFACEBOOK
Image captionMwanamuziki wa bongo fleva Profesa Jay
Msanii wa bongofleva Joseph Haule maarufu kwa jina 'Profesa Jay' alipata ubunge wa jimbo la Mikumi mkoani Morogoro tangu mwaka 2015 mpaka sasa.
Profesa Jay alipata wadhfa huo baada ya kutoa wimbo wake uliotamba wa 'Ndio mzee'ambao ulikuwa unaeleza namna kiongozi anaweza kutoa ahadi bila kuzitimiza.
Msanii mwingine maarufu nchini humo ni Joseph Mbilinyi maarufu kama Mr.Two au Sugu amekuwa mbunge wa Mbeya mjini kupitia chama cha upinzani cha chadema nchini humo tangu mwaka 2010 mpaka sasa.
Mwaka 2018, Joseph Mbilinyi alishtakiwa kwa kumtumia lugha ya fedheha dhidi ya rais Magufuli na kutumikia kifungo cha miezi mitano.
Presentational grey line
MbungeHaki miliki ya pichaREUTERS
Huko nchini Uganda, msanii Bobi Wine ambaye jina lake asili ni Robert Ssentamu Kyagulani ni mbunge wa jimbo la Kyadondo mashariki,.
Bob Wine kwa sasa amekuwa mwiba mchungu kwa utawala wa rais wa Uganda, Yoweri Museveni, akiwa anakubalika na kuwavutia maelfu ya vijana ambao wanamuunga mkono.
Bob Wine alishinda kiti cha ubunge mwaka 2017 akiwa mgombea binafsi baada ya kutojiunga na chama chochote.
JOSEHaki miliki ya pichaFACEBOOK
Wakati Harmonise akisifiwa na rais wake baada ya kuimba wimbo wa kumsifu rais wake, msanii nyota nchini Uganda, Jose Chameleone ambaye jina lake halisi ni Joseph Mayanja aliyeongoza wanamuziki nyota nchini humo kumuimbia rais Mseveni wimbo wa kampeni wa 'Tubonga nawe' kumsifu rais wao mwaka 2015.
Lakini alipotangaza nia mwaka huu rais Museveni alijitoa urafiki na Chameleone katika kurasa wa Twitter.
Chameleone ambaye ni mmoja wa wanamuziki maarufu katika eneo la Afrika Mashariki.
Moja ya nyimbo zake zinazofahamika ni ule wa 'Shida za Dunia', unaozungumzia matatizo yanayowakabili watu.
Mwanamuziki huyo anayewania umeya wa mji wa Kampala alisema :"Wakati huduma zinapokuwa katika hali mbaya, watu wanaanza kuamka ...Watu wana kiu ya uongozi unaofaa na hawajaupata".
"Wale wanaodhani kuwa ni mkumbo wa Bobi Wine wana ukweli kiasi fulani ," Chameleone alinukuliwa akisema hayo mwanzoni mwa mwezi Juni.
JaguarHaki miliki ya pichaFACEBOOK
Huko nchini Kenya mwanamuziki Charles Njagua Kanyi maarufu kwa jina la Jaguar alishinda ubunge wa jimbo la Starehe jijini Nairobi kupitia tiketi ya chama tawala cha Jubilee mwaka 2017.
Jaguar ni mwanasiasa mwenye mvuto kwa vijana na wanawake nchini humo.
Hivi karibuni mwanamuziki huyo alishtakiwa kwa kutoa kauli ya chuki dhidi ya wafanyabiashara wa kigeni nchini humo.