VIGOGO sita wa Kampuni ya Six Telecom akiwemo Wakili  maarufu Dk. Ringo Tenga wamehukumiwa kulipa faini ya Sh.milioni 155 au kutumikia kifungo cha mwaka mmoja jela. Pia wamehukumiwa kulipa fidia ya dola za Marekani 3,748,751.19 ambayo ni sawa na takribani Sh.milioni nane za Tanzania

VIGOGO sita wa Kampuni ya Six Telecom akiwemo Wakili  maarufu Dk. Ringo Tenga wamehukumiwa kulipa faini ya Sh.milioni 155 au kutumikia kifungo cha mwaka mmoja jela. 

Pia wamehukumiwa kulipa fidia ya dola za Marekani 3,748,751.19 ambayo ni sawa na takribani Sh.milioni nane za Tanzania

Aidha washitakiwa hao kila mmoja ametakiwa leo leo kulipa dola 150,000 kila mmoja mbayo tayari  wameishalipa. Pia Mahakama imeamuru kutaifishwa kwa nyumba ya washitakiwa iliyopo Mikocheni kiwanja Namba 33 yenye  thamani ya zaidi ya Sh.bilioni moja.

Mbali na Tenga, washitakiwa wengine waliohukumiwa ni Hafidhi Shamte au Rashidi Shamte ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa kampuni wa hiyo, mfanyabiashara na Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Peter Noni, Mkuu wa fedha wa kampuni hiyo Noel Chacha, Kampuni ya Six Telecoms na Frank Mwalongo.

Akisoma adhabu hiyo leo Oktoba 7,mwaka 2019 Hakimu Simba amesema katika kosa la kwanza, mshitakiwa wa kwanza hadi watano, atatakiwa kulipa faini ya Sh.milioni 10 kila mmoja au kifungo cha miezi 10, katika shtaka la pili washtakiwa hao watatakiwa kulipa faini ya Sh milioni 10 au kifungo miezi 12.

Katika shtaka la tatu, washitakiwa wametakiwa kulipa faini ya Sh.milioni tano au kifungo cha miezi 12 huku katika shtaka la nne watatakiwa kulipa faini ya Sh.milioni tano.

Aidha, Hakimu Simba ametoa amri sita ikiwemo washitakiwa kulipa fidia ya dola 3,748,751.19, washitakiwa kulipa dola 150,0000 na kiasi kilichosalia ambazo ni dola  3,581,115 ilipwe ndani ya miezi sita kuanzia leo.

Pia amesema, mshitakiwa wa sita ambaye ameunganishwa katika kesi hiyo atatakiwa kulipa faini ya Sh.milioni 30.Hakimu Simba amesema, endapo washitakiwa watashindwa kufanya hivyo DPP anamlaka ya kuchukua hatua za kisheria .

Mapema kabla ya kusomwa kwa adhabu hiyo, Wakili wa Serikali Mkuu Faraja Nchimbi alidai washtakiwa hao ni wakosaji wa kwanza kwani hawana kumbukumbu ya makosa ya nyuma ya washitakiwa,.pia ameiomba Mahakama katika kutoa adhabu, ifikirie kutoa adhabu chini ya kifungu cha 194 cha Sheria namba 4 ya 2019 ikizingatia makubaliano waliyoingia kati ya upande wa mashitaka na washitakiwa na kusajiliwa katika mahakama hiyo.

Alidai Mahakama itoe amri kwa washitakiwa kulipa fidia ya Dola za Marekani 3,748,751.19 na mshitakiwa wa kwanza hadi wa tano, walipe leo fidia ya Dola za Marekani 150,000 na wakubali kukabidhi nyumba iliyopo Mikocheni jijini Dar es Salaam

Pia alidai mshitakiwa wa kwanza hadi wa tano atatakiwa kulipa fedha zilizobaki kwa miezi sita kuanzia tarehe ya leo huku pia wakiiomba mahakama kuamuru mshitakiwa wa sita kulipa Sh.milioni 30 kama hasara aliyosababisha kwa Serikali.

Wakili wa utetezi Alex Mgongolwa amedai washitakiwa hao ni wakosaji wa kwanza na kwamba kumbukumbu zinaonesha kuwa hatima ya shauri hilo imetokana na sheria hiyo.Hivyo aliiomba Mahakama ijikite kwenye makubaliano katika kutoa adhabu kama yalivyosajiliwa mahakamani hapo.

"Mashitaka yote yanatoa uchaguzi wa adhabu ya faini hivyo, tunaomba mahakama iwape adhabu nyepesi," alidai Mgongolwa.Kwa mara ya kwanza washitakiwa hao walifikishwa mahakamani Novemba 20,2017.

Washitakiwa hao wanadaiwa kuwa  kati ya Januari 1, mwaka 2014 na Januari 14,mwaka 2016 maeneo ya Dar es Salaam, walitoza malipo ya mawasiliano ya simu za kimataifa chini ya kiwango cha Dola za Marekani 0.25 kwa dakika kwa lengo la kujipatia faida.

Pia katika kipindi hicho, wanadaiwa kuhujumu miundombinu ya Mamlaka ya Mawasiliano nchini(TCRA) kwa kutoza gharama chini ya kiwango na kushindwa kulipa kiasi cha Dola za Marekani 3,282,741.12 kwa TCRA, kama malipo ya mapato na kushindwa kulipa ada za udhibiti za dola  466,010.07 kwa TCRA.

Pia washitakiwa hao wanadaiwa kuwa waliisababishia TCRA hasara ya dola  3,748,751.22 ambazo ni sawa na Sh. bilioni nane.