IKIWA ni siku mbili baada ya tangazo la nia ya wawili hao kujitoa katika nafasi zao kama wanafamilia waandamizi wa familia ya kifalme ya Uingereza walilolitoa usiku wa Jumatano ya Januari 8. 2020, Meghan Markle, mke wa Mwanamfalme Harry ameondoka nchini Uingereza kwenda nchini Canada.
Awali Meghan alikuwa muigizaji nchini Marekani na moja kati ya kazi zake maarufu ni kucheza nafasi ya mwanasheria kwenye tamthilia ya “Suits”. Aliishi Canada ambapo pia inasemekana hata kupindi cha likizo ya Krismasi yeye, mumewe na mwanaye walikuwa nchini humo lakini mwanaye aliachwa nchini humo baada ya wawili hao kurudi Uingereza.
Hata hivyo, taarifa zinadai kuwa Harry amebaki Uingereza ili aongoze droo ya Kombe la Dunia ya ligi ya Raga itakayofanyika Buckingham, Uingereza.
Hii itakuwa mara ya kwanza kwake kuonekana hadharani baada ya kutoa tangazo lililoitikisa familia ya kifalme.
Uamuzi wa wawili wao kujitoa katika shughuli za kifalme kama wanafamila wandamizi wa familia hiyo, umepewa jina maarufu la Megxit ikiwa kama kashfa juu ya Megan ambaye analaumiwa kwa kumsukuma Harry kuridhia kitendo hicho cha kujiondoa kwa kutumia njia zake za “ki-California”.
Vyombo vya habari vya Uingereza, hasa vile vinavyofuatilia na kuiunga mkono familia ya kifalme, vimemshutumu Megan kwa kusababisha mfarakano ndani ya familia hiyo. Shutuma zingine zimewataja wawili hao kuwa wabinafsi kwa kujali furaha yao na kujiridhisha wao wenyewe bila kutazama mbali zaidi ya matakwa yao wenyewe.
Vyombo vya habari navyo vililaumia na Harry na mwenzi wake huyo mnamo Oktoba 2019 baada ya kumfuatilia sana Megan na hata kuharibu wasifa wake na kuingilia mambo yake binafsi. Hatua hii inahisiwa kuwa moja ya sababu zinazoaminiwa kuchochea uamuzi huo kufikiwa na wawili wao.
Harry ni mhanga mmojawapo wa ufuatiliaji wa kukithiri wa vyombo vya habari kwani mama yake, marehemu Diana, alifuatiliwa mpaka akafa katika ajali akiwa anawakimbia waandishi wa vyombo vya habari mnamo mwaka 1997.
0 Comments