Sherehe za maadhimisho ya miaka 56 ya Mapinduzi ya Zanzibar zimefanyika leo Jumapili Januari 12, 2020 katika Uwanja wa Abeid Aman Karume.
Viongozi mbalimbali wamehudhuria maadhimisho hayo ya Mapinduzi ya Januari 12 mwaka 1964 na mgeni rasmi ni Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein.




Baadhi ya viongozi waliohudhuria ni; Rais wa Tanzania, John Magufuli, Makamu wake, Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi na Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa.
Pia, Marais wastaafu wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa, Jakaya Kikwete na Rais mstaafu wa Zanzibar, Aman Abeid Karume.
Mawaziri wakuu wastaafu wa Tanzania, Edward Lowasa na Frederick Sumaye nao wamehudhuria sherehe hizo.
Wengine ni, Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma na Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omary Othman Makungu na wakuu wa vikosi vya ulinzi na usalama.
Rais Shein amewasili uwanjani hapo akitumia gari maalumu la wazi akizunguka uwanjani kusalimiana na mamia ya wananchi waliojitokeza.
Kisha alifika eneo maalum lililotengwa kwa ajili ya wimbo wa Taifa la Zanzibar ule wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliokwenda sambamba na kupigiwa mizinga 21.
Badaye Rais Shein alipata fursa ya kukagua gwaride maalum la vikosi vya ulinzi na usalama na akarejea kukaa jukwaa kuu kwa ajili ya kupokea maandamano ya wananchi kutoka mikoa yote mitano ya Zanzibar.
Maandamano hayo yanawakilisha wafanya kazi wa taasisi mbalimbali za Serikali pamoja na wanafunzi wa vyuo vikuu.
Baadhi ya waandamanaji hao waliojawa na bashasha wamepita mbele ya jukwaa kuu wakiimba nyimbo za hamasa zilizobeba kauli mbiu mapinduzi daima ‘’tutayalinda na kuyatunza potelea mbali’.’

Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli anaashiriki sherehe za Maadhimisho ya miaka 56 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar zinazofanyika katika uwanja wa Amaan.