Kundi la kigaidi la Al Shabaab limefanya shambulio katika uwanja wa ndege wa jeshi unaotumiwa na majeshi ya Marekani na Kenya eneo la Lamu, kusini mashariki mwa Kenya.
Kundi hilo la kigaidi la mtandao wa Al-Qaeda limesema kuwa tukio hilo halina uhusiano wowote na malumbano yanayoendelea kati ya Iran na Marekani.
Jeshi la Kenya limethibitisha kutokea kwa shambulio hilo katika uwanja wa ndege wa Lamu.
Msemaji wa jeshi la Kenya amesema kuwa wameweza kudhibiti shambulio hilo na wamekuta miili minne ya wanamgambo wa Al Shabaab.
Al Shabaab walikuwa wanajaribu kuelekea kambi ya karibu inayotumiwa na Marekani na jeshi la Kenya.
Wakazi wa eneo hilo wameripoti kuwa walikuwa wanasikia milipuko na baadae milio ya risasi.
Moshi mzito ulionekana katika eneo la tukio.
Uwanja wa ndege wa Lamu umefungwa kwa muda usiojulikana.
Mashambulizi hayo yamesababisha madhara kiasi gani?
Taarifa zinasema kuwa ndege mbili , helkopta mbili na magari kadhaa yaliharibiwa katika shambulio hilo.
Al-Shabab walidai kuwa kuna vifo vingi na majeruhi wa vikosi vya Marekani na wanajeshi wa Kenya hapo.
Jambo ambalo Christopher Karns, msemaji wa Kitengo cha Jeshi la Marekani Afrika amekanusha taarifa hizo na kusema kuwa huo ni uzushi wa kukuza mambo.
Aidha hakufafanua zaidi taarifa hizo, AP imeripoti.
Kambi hiyo ilikuwa na wamarekani wapatao 100.
Ikumbukwe kuwa mwezi Juni 2018, Komando wa Marekani aliuwawa nchini Somalia wakati wa shambulio la al-Shabab.
Marekani ilianza operesheni dhidi ya wanamgambo tangu rais Donald Trump aingie madarakani 2017.
Marekani ilifanya mashambulizi mengi zaidi ya anga nchini Somali mwaka 2019 zaidi ya miaka ya nyuma.
Hali ya kiusalama katika fukwe za Manda ni imara.
Siku mbili zilizopita kundi la kigaidi la Al-Shabaab lilihusika na mauaji ya watu watatu katika basi katika eneo la Lamu.
Na wiki iliyopita kundi hilohilo la kigaidi lilihusika na shambulio lililouwa zaidi ya watu 80 huko Mogadishu.
|
0 Comments