WAZIRI wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu anatarajiwa kuzindua mashine mpya ya CT Scan katika Hospitali ya Kilutheri Ya Haydom iliyoko wilayani Mbulu mkoani Manyara mnamo Januari 15, mwaka huu siku ya Haydom Day.


CT Scan ni mashine ambayo inatumika katika kufanya vipimo vya mionzi vya uchunguzi katika mwili wa binadamu ili kubaini matatizo ambayo hayakuweza kuonekana kwa vipimo vingine ambapo vipimo ivyo ni kama vya viungo (organs), mifupa (bones) na nyama (tissues).


Mashine ya CT Scan ya Hospitali ya Kilutheri ya Haydom imepatikana baada ya uongozi wa hospitali hiyo kufanya changizo kwa wadau mbalimbali nchini na kwa kupitia mbio za Haydom Marathon za km 21, km 10 na km 5 fun zilizofanyika mwaka 2018 ili kupata shilingi milioni 800 ya kununulia CT Scan mpya baada ya waliyokuwa nayo awali kuharibika mwaka 2017.

Mkurugenzi mtendaji wa tiba Hospitali ya Kilutheri ya Haydom, Dkt. Emanuel Q. Nuwass amesema maandalizi yanaendelea vyema wanatarajia mgeni rasmi siku ya uzinduzi atakuwa waziri wa afya maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto Ummy Mwalimu na kuweka wazi kuwa lengo lao ni kuendelea kuboresha huduma za afya katika kituo chao kuanzia ngazi ya chini hadi rufaa.

Amesema mbali na mashine ya CT Scan maboresho mengine waliyofanya ni ununuzi wa vifaa vingine tatu ambazo sasa inazifanya kuwa nne vipya na yote ni kwa matumizi ya hosipitali pia upanuzi na uboreshaji wa mazingira ya hospitali ili yafae kupokea vifaa hivyo ikiwemo idara ya mionzi.

Amezitaja vifaa hivyo kuwa ni Digital X-Ray, mashine ya kuzalisha Oxygen kwa ajili ya wagonjwa (oxygen plant) na mashine ya kisasa ya kuchoma na kuteketeza taka hatarishi za hospitali (Incinerator) ambapo pamoja na mashine ya CT Scan zote zimegarimu kiasi cha shilingi bilioni 1,512.3 huku uboreshaji wa miundombinu ikigharimu shilingi milioni 91.2.



Amesema baadhi ya changamoto waliyokuwa wanakumbana nayo baada ya CT Scan ya awali kuharibika mwaka 2017 ilikuwa ni wagonjwa kupata adha ya kupewa rufaa ya kwenda vituo vya mbali na wengine walikuwa wanashindwa kwenda huko, kutokana na uwezo wao kuwa mdogo kiuchumi.

Ameongeza kuwa kulikuwa na wagonjwa ambao walikuwa wanapoteza maisha kwa kuwa walikuwa wanakuwa katika hali mbaya ambayo hawawezi kupewa rufaa na kwa wakati huo hauwezi kujua tatizo lao ni nini ili kuweka kuwasaidia.


Katika hatua nyingine, Dokta Nuass amesema tayari bodi yao imepitisha azimio la kufanya mbio kuwa moja ya mbinu ambazo zinawasaidia kukutana na wadau wengi wakiwemo wananchi katika kuchangia maboresho ya huduma za afya kwa iyo mbio za Haydom Marathon zitakuwa ni endelevu.
Na Kennedy Lucas, Manyara.