Kenya na Nigeria ni miongoni mwa nchi ambazo raia wake wana imani na Rais Donald Trump wa Marekani, kulingana na kura ya maoni iliyofanywa na kituo cha Pew Research Center.
Kura hiyo ya maoni iliyolenga kubaini fikra za watu kumhusu Trump na uongozi wake, ilionesha kwamba asilimia 65 ya raia wa Wakenya wana imani na kiongozi huyo wa Marekani, huku aslimia 58 ya raia wa Nigeria wakiunga mkono uongozi wa Trump.

Hilo linawadia licha ya hatua za awali ambazo hazikuendana na baadhi ya mataifa ya Afrika, ikiwemo kusema mara kadhaa kwamba "Nchi za mataifa ya Afrika ni machafu".
Mataifa hayo mawili ni miongoni mwa mengine 33 ambayo kura hiyo ya maoni ilifanyika kati ya mwezi Mei na Oktoba mwaka 2019.
Kituo cha utafiti cha Pew pia kilibaini kwamba mataifa yaliyoko kusini mwa jangwa la Sahara yameonyesha kumpenda Rais Trump.
Kenya na Nigeria ni miongoni mwa nchi zinazopokea msaada mkubwa wa kiuchumi kutoka kwa Marekani kulingana na shirika la linalofuatilia masuala ya usalama lenye mamako yake Marekani la Security Assistance Monitor.
Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari alikuwa rais wa kwanza wa Afrika kualikwa katika Ikulu ya Marekani mwaka 2018.
Utawala wa Trump pia uliiuzia Nigeria ndege 12 za kivita za Marekani kinyume na ilivyokuwa sera ya enzi ya wakati wa Rais Obama.
Pia unaweza kusoma:

Maoni kumhusu Trump

Asilimia 29 pekee ya nchi zilizofanyiwa kura hiyo ya maoni , zilionyesha kuwa na Imani na Trump kulingana na vile uongozi wake umeuwa tangu mwaka 2017.
Shirika la Pew limesema kwamba idadi ndogo ya watu wenye Imani naye inatokana na kupinga sera ya mambo ya nje ya Trump
Sera ya Trump kuhusu kodi, uhamiaji na msimamo wake kuhusu Iran ni miongoni mwa yalichongia kupata uungwaji mkono mdogo.
Aidha majadiliano yake na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un kulimfanya kuungwa mkono zaidi katika nchi zote 33 zilizohusika katika utafiti huo.

Wanaompendelea Trump

Nchini Marekani, Shirika la Pew lilibaini kwamba kiujumla Trump bado anapendwa duniani.
"kura ya maoni inayoonesha kumuunga mkono Trump ilishuka kwa kasi baada tu ya kuingia madarakani na pia bado umaarufu wake ulishuka zaidi ikilinganishwa na enzi ya Rais Obama," kulingana na shirika la Pew.
Hata hivyo mwaka jana, idadi ya wanaompenda Trump ilianza kuongezeka na pengine hilo lilisababishwa na hatua yake ya kuanza kuunga mkono wafuasi wa mrengo wa kulia katika baadhi ya mataifa.
Kiujumla, Israel ndiyo iliyokuwa na idadi kubwa ya raia wanaompendelea Trump ikiwa ni asilimia 83, kwa mujibu wa Shirika la Pew.
Mexico, Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini, maoni kumhusu Trump yalionyesha kupinga utawala wake tena kwa kiasi kikubwa huku nchini Uturuki mtu mmoja tu kati ya watano akionyesha kuipendelea Marekani.