Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta na mwenyeji wake Donald Trump wa Marekani wamekutana na kuratibu majadiliano ya mkataba wa biashara huru kati ya mataifa hayo mawili.
Mkataba huu utakuwa ni wa kipekee kuwahi kufanywa kati ya Marekani na taifa la bara Afrika, na rais Kenyatta amesema kuwa mkataba huu mpya hautaathiri mkataba wa soko huru la Afrika (AfCFTA) ambao utaanza kutekelezwa Julai mwaka 2020.

Saa chache kabla ya marais Kenyatta na Trump kukutana, waziri wa uchukuzi nchini Kenya James Macharia ambaye pia yuko Marekani alishiriki katika uwekaji saini wa mkataba wa usafiri wa anga ulioratibiwa, ambao unahusu uchukuzi wa mizigo au bidhaa.
Rais Uhuru kenyatta pamoja na mawaziri mablimbali wa Kenya wakiwa katika kikao na raia Donald Trump MarekaniHaki miliki ya pichaIKULU YA RAIS KENYA
Image captionRais Uhuru kenyatta pamoja na mawaziri mablimbali wa Kenya wakiwa katika kikao na raia Donald Trump Marekani
Mkataba huu unatoa nafasi kwa makampuni ya ndege kutoka nchi zote mbili kuanzisha na kuendesha oparesheni za kusafirisha bidhaa moja kwa moja kati ya Kenya na Marekani.
Kenya ni moja kati ya mataifa 38 yanayofaidika na mpango wa Marekani wa African Growth and Opportunity Act ama AGOA, ambao unaruhusu zaidi ya bidhaa 6,500 kutoka mataifa ya Afrika kuingizwa Marekani bila kutozwa ushuru.
Onesmus Masinde ambaye ni mkuu wa biashara, utafiti na sera katika Chama cha wafanyabiashara nchini Kenya (KNCCI) amesema mkataba huu utachangia katika ukuaji wa uchumi, na kwamba hautasambaratisha mkataba wa Agoa ambao unafikia kikomo mwaka 2025.
''Mkataba huu unaipa Kenya fursa ya kufanya biashara zaidi ya masharti ya Agoa. Hii ni kwasababu Agoa inagusia mambo machache tu, kama vile orodha ya bidhaa zinazofaa kuingia marekani bila ushuru, lakini sasa mkataba huu una upana zaidi, na ni baina ya nchi kwa nchi,'' alisema Masinde.
Rais Uhuru Kenyatta na mwenzake wa Marekani Donald Trump pamoja na mawaziri wao katika kikao kilichofanyika ikulu ya Whitehouse MarekaniHaki miliki ya pichaIKULU YA RAIS KENYA
Image captionRais Uhuru Kenyatta na mwenzake wa Marekani Donald Trump pamoja na mawaziri wao katika kikao kilichofanyika ikulu ya Whitehouse Marekani
Wadadisi wanahoji kuwa mkataba huu ungekuwa na uzito zaidi iwapo mataifa ya Afrika yangejadiliana na Marekani kwa pamoja, badala ya kufanya mazungumzo kati ya nchi kwa nchi. Masinde ana mtazamo tofauti.
''Kuna changamoto ikiwa tutajumuisha nchi zote kwa mazungumzo kwani kutakuwa na kuchelewa, kuchukua muda kukubaliana ni mambo gani tunapendekeza, na pia uchumi wan chi husika unatofautiana, kuna wengine watahitaji kuwekewa vikwazo…ikiwa tutaenda kama jumuiya kutakuwa na kuvutana, '' aliongezea Masinde.
Mwaka 2018, Kenya ilisarifisha bidhaa za thamani ya $644 milioni hadi Marekani; miongoni mwa bidhaa hizo zikiwa ni kahawa na mafuta.
Rais Uhuru Kenyatta na rais Donald Trump wakati wa mkutano wa kibiashara kati ya mataifa hayo mawiliHaki miliki ya pichaIKULU YA RAIS KENYA
Image captionRais Uhuru Kenyatta na rais Donald Trump wakati wa mkutano wa kibiashara kati ya mataifa hayo mawili
Mwaka huo huo, Marekani ilisafirisha bidhaa za thamani ya $365 milioni hadi Kenya - mitumba, kemikali, mashine za kilimo, miongoni mwa bidhaa zingine.