KOCHA Mkuu wa Yanga, Luc Eymael amepanga kumpa darasa zito kipa wake, Metacha Mnata kwa kumuweka chini na kutazama marudio ya mechi dhidi ya Lipuli FC na kuangalia namna alivyoruhusu bao wakati wa mechi hiyo ya Ligi Kuu Bara, juzi Jumatano.
Kocha huyo raia wa Ubelgiji amepanga kumpa darasa hilo Metacha kwa kuutazama mchezo huo baada ya kuona kipa huyo hakukaa katika eneo lake wakati ambao alipigiwa faulo iliyozaa utata baada ya mpira aliopigiwa kuingia ndani ya goli.
Katika mechi hiyo Metacha alipigiwa faulo ya moja kwa moja na Kenneth Masumbuko wa Lipuli katika dakika ya 52 na mpira ambao aliutema ukaelekea langoni kwake, aliudaka lakini ulizua utata mkubwa kama ulivuka mstari au la, baadaye mwamuzi akaamuru iwe kona.
Eymael amesema kuwa atampa darasa hilo Metacha kutokana na kuona kipa huyo hakujipanga sawasawa ambapo ameona hayo kwa sababu yeye alikuwa kipa wakati anacheza soka.
“Tunatakiwa kuangalia marudio ya mechi hii na Lipuli hasa kwa sababu kulikuwa na makosa ya kipa kujipanga wakati wa faulo ile ilipopigwa.
“Nafikiri mpira ulikuwa ndani na mimi kama kipa mstaafu baada ya mechi kumalizika nilimwambia juu ya hilo lakini tutakaa tena na kuangalia tena bao lile jinsi lilivyokuwa,” alisema Eymael.
0 Comments