WIZARA ya Mambo ya Ndani ya Nchi, imetangaza ajira zaidi ya 4,400 kwa vyombo vya ulinzi na usalama nchini. Akiwasilisha makadirio ya bajeti ya mwaka 2020/21, Waziri wa wizara hiyo, George Simbachawene, alisema ajira hizo zitakwenda pamoja na mafunzo mbalimbali kwa askari na watumishi mbalimbali.
Alisema kwa mwaka huo, Jeshi la Polisi linatarajia kuajiri askari 2,725, askari Magereza 685, Uhamiaji 495 na Zimamoto 501.
Simbachawene alisema katika mwaka 2020/21 Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wadau wa ndani na nje ya nchi limepanga kuendelea kutoa mafunzo mbalimbali kwa maafisa, wakaguzi na askari 9,465 pamoja na watumishi raia 25.
Alisema kati ya hao 9,051 watapata mafunzo ndani ya nchi kupitia vyuo vya polisi na 414 nje ya nchi kwa udhamini wa taasisi na nchi mbalimbali.
Aidha, alisema katika kuimarisha kuimarisha utendaji kazi wa watumishi wa Jeshi la Polisi jumla ya maofisa, wakaguzi, askari na watumishi raia 5,470 wamepata mafunzo mbalimbali, kati ya hao 5,461 walipata mafunzo ndani ya nchi na tisa nje ya nchi.
Kwa upande wa Jeshi la Magereza, alisema katika kipindi cha Julai,2019 hadi Machi, 2020 jumla ya maofisa naaskari 1,537 walipata mafunzo ya uongozi wa kijeshi katika Vyuo vya Magereza nawatumishi 951 walihitimu mafunzo ya taaluma mbalimbali katika vyuo vya ndani na nje ya Jeshi.
“Jeshi linatarajia kuajiri askari 685 wenye fani mbalimbali watakaopatiwa mafunzo ya awali katika Chuo cha Magereza Kiwira (Mbeya), mafunzo ya uendeshaji wa Magereza na Taaluma ya Urekebishaji kwa Maafisa na Askari 3,270 katika ngazi mbalimbali za uongozi,” alisema.
Waziri Simbachawene alisema kuhusu hali ya ulinzi na usalama magerezani, hadi kufikia mwezi Machi, 2020 kulikuwa na jumla ya wafungwa na mahabusu 32,438 katika magereza yote nchini na kwamba kati ya hao, wafungwa ni 14,464 na mahabusu 17,974 ambapo ni asilimia 9 zaidi ya uwezo uliopo wa kuhifadhi wafungwa na mahabusu 29,902.
Simbachawene alisema mwaka 2020/21Idara ya Uhamiaji inatarajia kuajiri askari 495 na kuwapa mafunzo ya awali, ikiwamo kuendelea kutoa mafunzo mbalimbali kwa maofisa, askari na watumishi raia ili kuwaongezea ujuzi wa utendaji kazi kwa ufanisi zaidi.
Alisema katika kukabiliana na changamoto ya upungufu wa rasilimaliwatu, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji linatarajia kuwapandisha vyeo Maoafisa na askari 1,311 na kuajiri askari wapya.
0 Comments