WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi ameliagiza jeshi la polisi nchini kuwa na mbinu za kistaarabu za kisimamia sheria za usalama barabarani na kuacha kujificha na kuwashtukiza madereva wanaoendesha magari kwa mwendokasi.
Ameyasema hayo bungeni mjini Dodoma wakati akiwasilisha makadirio ya matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2020/2021, ambapo amesema vitendo vya polisi kujificha na kuvizia magari, vinaweza kusababisha polisi wenyewe kugongwa.

“Kwanini tujifiche? Maana barabarani tupo kila siku, na sisi ndiyo madereva, sioni sababu ya kujificha. Spidi ziko barabarani mle, tuendelee kuongeza elimu zaidi kwa madereva wetu wapate uelewa na kufuata alama za barabarani,” amesisitiza.
Aidha, amemugiza Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Simon Sirro kutoa maelekezo maalum juu ya udhibiti wa mwendo wa barabarani kwa sababu kinachofanyika sasa kinaleta fujo.
Ameongeza kuwa utaratibu wa polisi kutumia simu kupiga picha magari yanayokwenda kasi haukubaliki kwa sababu kuna kifaa maalum cha kufanya kazi hiyo.
“Huyu ana Nokia, huyu ana iPhone, huyu ana Samsung, tunaaminianaje, kwamba ni kitendea kazi ambacho tumekipitishwa kisheria. Hii haikubaliki,” amesema.