Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, Harold Wilson, alipata kutoa kauli ambayo imekuwa ikirudiwa kwenye matukio tofauti tangu mwenyewe aitoe katikati ya miaka ya 1960. Maneno yalikuwa; "Wiki moja ni muda mrefu katika siasa".
Katika kipindi cha wiki moja iliyopita, Paul Makonda alikuwa Mkuu wa Mkoa na Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Dar es Salaam.
Alikuwa mmoja wa watia nia ya ubunge katika Jimbo la Kigamboni na kulikuwa na maneno kwamba alikuwa mbioni kukabidhiwa wadhifa mkubwa endapo atashinda kinyang'anyiro hicho.
Leo asubuhi, ndani ya wiki hiyo moja, Makonda ameamka akiwa hana cheo chochote.
Si Mkuu wa Mkoa na ameshindwa katika kura za maoni Kigamboni. Vikao vya juu vya chama vinaweza kuamua kurudisha jina lake ingawa jambo hilo linaweza kuwa gumu kwa sababu litaibua mgawanyiko ndani ya chama.
Katika uchaguzi huo wa Kigamboni, Makonda alipata kura 122 huku mshindi; Dk. Faustine Ndugulile, aliyepata kuwa Naibu Waziri wa Afya kwenye serikali ya Rais John Magufuli, akimshinda kwa kupata kura 190.

Kipenzi cha Rais

Kumekuwapo na dhana kwamba Makonda ni kipenzi cha Rais. Mfano mashuhuri unaotumiwa na wengi unahusu sakata la vyeti. Serikali ya Rais Magufuli inajulikana kwa suala la kufukuza kazi watumishi wa serikali waliokuwa na vyeti feki au mushkeli kwenye elimu.
Wakati maelfu ya watumishi wa serikali wakifukuzwa kazi, kuliibuka tuhuma kwamba Makonda pia alitumia vyeti vya kielimu visivyo vyake na hivyo alitakiwa kuchukuliwa hatua kama wenzake hawa. Ndiyo wakati kuliibuka maneno kwamba jina lake halisi ni Daudi Albert Bashite.
Hata hivyo, hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa dhidi yake. Makonda pia amewahi kutoa kauli tata zilizowahi kuitia Tanzania matatani katika Jumuiya ya Kimataifa kama msimamo wake kuhusu suala la ushoga lakini bado akaendelea kubaki kwenye nafasi yake.
Swali kubwa ambalo limekuwa likiulizwa hadi sasa na mabalozi na wadau wengine wa Jamii ya Kimataifa lilikuwa moja tu; Makonda ni nani kwa Rais? Hadi leo, hakuna ambaye amewahi kulijibu swali hilo kwa ufasaha.

Huu ni mwisho wa Makonda?

Katika umri wa miaka 38 alionao sasa, ni mapema kuanza kuandika tanzia ya maisha yake ya kisiasa kwa sababu ya kushindwa kwenye mchakato wa ubunge wa Kigamboni na kuondolewa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Nimemfahamu Makonda kwa kipindi kirefu tangu akiwa mwanafunzi wa Chuo cha Ushirika Moshi na katika siku zake za mwanzoni kwenye siasa na ninafahamu kwamba ni mpambanaji aliye tayari kufanya chochote kutimiza lengo lake.
Katika duru za kiutawala ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikalini, kuna jambo limeanza kufahamika na linazungumzwa kwa kificho; kwamba katika mojawapo ya madhaifu ya Rais Magufuli mojawapo ni huruma kwa wasaidizi au watendaji wake pale wanapomwomba msamaha kwa dhati kabisa.
Pasi na shaka yoyote, Makonda analijua hili na atafanya kila linalowezekana ili aweze kupata huruma ya Rais. Kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania, Rais kama Mkuu wa Nchi na Serikali ana mamlaka makubwa ya uteuzi na ziko nafasi nyingi za kumteua kama ataona zitafaa.
Zipo taarifa za viongozi walioondolewa madarakani kwa tuhuma nzito lakini sasa wamerejeshwa ama kwa sababu imebainika kulikuwa na 'chumvi' kwenye tuhuma hizo au wakosaji wamekiri makosa, kuomba radhi na kuonyesha wako tayari kufanya chochote kumuunga mkono Rais.
Makonda ameshindwa tu katika mchakato wa uchaguzi na ingawa wapo viongozi wa CCM ambao walionya kuhusu viongozi wa serikali waliokuwa na vyeo tayari kwenda kuwania ubunge; ni vigumu kumhukumu mwanasiasa kwa kosa la tamaa ya madaraka.
Tamaa hii ya madaraka ndiyo huwaamsha wanasiasa kila asubuhi kwenda kwenye shughuli zao.
Taarifa aliyoitoa kupitia mtandao wa Instagram leo kuhusu kilichotokea inatoa picha kwamba ingawa amekubali matokeo, bado anaamini ana maisha katika siasa. Taarifa hiyo ina maneno kama "ndoto" na "Mipango ya Mungu" ambayo kihalisia huwa haina muda wa kumalizika.

Makonda na Katiba ya Warioba

Tukio moja lililomtambulisha Makonda kwa Watanzania ni lile lililohusu namna alivyomshambulia hadharani Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba, aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya kutafuta maoni ya Katiba mpya ya Tanzania.
Makonda, wakati huo akiwa hana wadhifa wowote serikalini, alikuwa akipinga baadhi ya mapendekezo ya Tume ile na bila shaka alikuwa amepewa maelekezo ya kufanya hivyo na baadhi ya waliokuwa vigogo wa CCM wakati ule.
Ingawa wapo walioona kitendo kile kama ukosefu wa adabu mbele ya wazee, Makonda aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya na Rais Jakaya Kikwete na baadaye Magufuli akampandisha cheo na kuwa Mkuu wa Mkoa.
Kwa hali ilivyo sasa, Makonda itabidi arudi kuwa Makonda aliyekuwa kabla hajawa Mkuu wa Mkoa au Wilaya. Atashambulia wapinzani wa CCM na kupongeza kwa nguvu zote kile kinachofanywa na serikali. Kwa sababu ya mahusiano yake mazuri na baadhi ya vyombo vya habari, atavitumia kufanya propaganda zake.
Miezi michache iliyopita, mtu angeweza kuandika kuhusu tanzia ya kisiasa ya aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba, ambaye aliondolewa madarakani na Rais Magufuli.
Baada ya kuendelea kupambana na kutetea serikali bila ya kuchoka, Mwigulu leo ni waziri tena katika serikali ya rais huyohuyo 'aliyemtumbua'.
Kama Makonda ni mwanafunzi mzuri wa siasa za Tanzania za sasa, anajua nini cha kufanya kuweza kurejea kwenye ulingo wa siasa za nchi. Kwa bahati nzuri, hizo ni aina ya siasa ambazo yeye alizifanya kabla ya wakati wake. Anazijua, anazielewa na amewahi kuzifanya huko nyuma.

Makonda na uvuvi

Historia ya Makonda ilibadilika wakati alipojiunga na Chuo cha Masuala ya Uvuvi, Mbegani, Bagamoyo na kukutana na Benjamin Sitta -mtoto wa aliyekuwa Spika wa Bunge la Tanzania, Samuel Sitta. Mtoto huyu ndiye aliyemkutanisha na babaye na baada ya hapo Makonda amefikia alipofikia.
Makonda ni kizazi cha wanasiasa ambao hawajawahi kufanya kazi yoyote kwenye maisha yao kuondoa siasa tangu walipomaliza masomo yao. Lakini angalau amesomea uvuvi na kwenye masomo hayo ndiko safari yake ya kisiasa ilipoanzia.
Katika uvuvi, Walatini wana dhana moja ambayo huirudia mara kwa mara; Duc in altum kwamba twekeni mpaka kilingeni. Inatokana na hadithi ya kwenye Biblia kati ya Yesu na Petro wakati akipewa kazi ya Utume.
Unapotweka wavu wakati wa kuvua samaki, unatakiwa utafute palipo na maji mengi. Paulo, jina la mmoja wa mitume wa Yesu, anajua nini cha kufanya kutoka alipo sasa.