Donald Trump alivaa barakoa kwa mara ya kwanza mbele ya umma Jumamosi iliyopita
Rais wa Marekani Donald Trump ameapa kutolazimisha Wamarekani kuvaa barakoa kama njia moja ya kudhibiti usambaaji wa virusi vya corona.
Maoni yake yanawadia wakati daktari mkuu nchini humo wa magonjwa ya kuambukiza, Dkt. Anthony Fauci, amesisitizia viongozi wa majimbo na maeneo kulazimisha raia kuvaa barakoa.
Kuvaa barakoa, Dkt Fauci ameongeza, ni muhimu sana na kila mmoja anastahili kuzitumia kila wakati.
Nchini Marekani kuvaa barakoa kumegeuka kuwa suala la kisiasa zaidi.
Magavana wengi wa majimbo, sasa wametoa agizo kwamba ni lazima kuvaa barakoa mtu anapotoka nje, wala sio hiari tena.
Miongoni mwao ni magavana wa Republican akiwemo Kay Ivey of Alabama,, ambaye amebadili msimamo wake wa awali na sasa amesema kuwa ni lazima kila mmoja kuvaa barakoa.
Rais Trump ambaye awali alikuwa anapinga uvaaji wa barakoa hata kwake binafsi, alivaa barakoa hadharani kwa mara ya kwanza Jumamosi iliyopita.
Lakini akizungumza na kituo cha habari cha Fox News Ijumaa, Bwana Trump alisema hakubaliani na suala la kulazimisha watu kuvaa barakoa akidai kuwa raia kwa kiwango fulani wanastahili kuwa na uhuru.
Mapema wiki hii, Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Marekani (CDC), kilitoa taarifa na kuasa kila mmoja kuvaa barakoa.
"Sio kwamba tumeshindwa kabisa katika vita dhidi ya COVID-19," Mkurugenzi wa CDC Dkt Robert R Redfield amesema. "Kujifunika nyuso ni moja ya silaha muhimu ya kupunguza na kusitisha usambaaji wa virusi, - hasa kila mmoja anapovaa katika ya jamii."
Coronavirus
Banner
Katika jimbo la kusini la Georgia, gavana wa Republican Brian Kemp amesisitizia raia kuvaa barakoa kufikia mwezi ujao.
Bwana Kemp alitoa ombo hilo kwa wakaazi licha ya kuchukua hatua ya kisheria siku moja kabla dhidi ya meya wa Atlanta, Keisha Lance Bottoms, kwa kufanya uvaaji wa barakoa kuwa lazima kwenye mji huo.
Bi. Bottoms yeye binafsi amepatikana na virusi vya corona.
Maafisa wa mji wa Oklahoma pia nao wanafikiria kufanya uvaaji wa barakoa kuwa lazima ikiwa jimbo halitachukua hatua.

Je ni majimbo gani yenye ongezeko la maambukizi?

Majimbo kadhaa Marekani yameathirika hasa ya kusini yanashuhudia ongezeko la juu la maambukizi yaliyothibitishwa ya virusi vya corona.
Mamia ya wahudumu wa afya wanajeshi wamepelekwa Texas na California kusaidia maafisa kukabiliana na maambukizi mapya ya virusi vya corona na Texas na Arizona, malori yenye majokofu yametumwa kuhifadhi miili ya waliokufa.
Wiki za hivi karibuni, hospitali zinazoshuhudia wagonjwa wengi kupita kiasi huko Florida pia nazo zimetoa taarifa kuwa vyumba vya wagonjwa mahututi vimejaa na hawawezi tena kukubali kupokea wagonjwa zaidi.
Dr Anthony Fauci
Maelezo ya picha,
Dkt Anthony Fauci amesema kuvaa barakoa ni muhimu
Katika baadhi ya miji na majimbo, yanawakati mgumu kukabiliana na ongezeko kubwa la wanaohitajika kupimwa virusi vya corona.
Huko Pittsburgh, Pennsylvania, watu wanaoshukiwa kupata maambukizi wameombwa kujitenga majumbani mwao kwa siku 14 badala ya kwenda kwenye vituo vilivyotengwa kupimwa, huku Hawaii bado inaendelea na kanuni yake ya kuweka wageni wote kwenye karantini kwa mwezi mmoja zaidi, kwasababu ya upungufu wa vifaa vya kupimia.

Vipi kuhusu shule?

Huku mamilioni ya watoto ikiwemo katika majimbo mawili maarufu ya Texas na California, wamearifiwa kwamba shule hazitafunguliwa kwa mwaka mpya wa masomo.
Elimu na suala la ni lini shule zinafunguliwa pia limegeuzwa kuwa la kisiasa.
Mwongozo mpya wa kufunguliwa kwa shule ulitarajiwa kutolewa wiki hii lakini vyombo vya habari vya Marekani vimeripoti kwamba umechelewa.
Marekani bado imesalia kuwa nchi yenye maambukizi ya juu ya virusi vya corona duniani.
Sasa hivi nchi hiyo imethibitisha maambukizi ya virusi vya corona milioni 3.6 na vifo zaidi ya 139,000 - idadi kubwa zaidi duniani.