ALIYEWAHI kuwa Mwenyekiti wa Klabu ya Simba, Ismail Aden Rage amefunguka kuwa, katu wasitokee watu wa kuicheka Yanga kutokana na ushindi wa bao moja katika kila mechi kwani wana uwezo wa kutwaa ubingwa kwa mabao hayohayo msimu huu.
Yanga ambayo ipo nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi kwa kushinda michezo mitatu kati ya minne iliyocheza kutokana na kutoa sare dhidi ya Tanzania Prisons, imejikuta ikipata ushindi wa bao moja katika kila mchezo.
Akizungumza na Championi Jumatano, Rage ambaye aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa FAT sasa TFF, amesema kuwa, Ligi ya safari hii ni ngumu na ina ushindani mkubwa kutokana na kila timu kufanya usajili mzuri, hivyo kusitokee mtu akabeza matokeo ya timu fulani.
“Ligi ni ngumu, kuna ushindani wa hali ya juu, timu zimejitahidi kufanya usajili mzuri na wachezaji wote wana majina hususani Simba na Yanga, hivyo kila timu inahitaji kupata matokeo mazuri ili kujiweka katika nafasi nzuri ya msimamo wa ligi.
“Hivyo asitokee mtu akabeza matokeo ya timu fulani, watu wanasema Yanga inashinda lakini mabao machache inapata bao moja katika kila mechi, wanaweza wakatwaa ubingwa na ushindi huohuo wa bao moja kwani hata Ulaya kuna timu ilitokea ilipata ubingwa kwa ushindi wa bao moja hivyohivyo hadi mwisho wa msimu, hivyo kila timu ipambane,” alisema Rage
0 Comments