USHINDI walioupata timu ya Yanga ya jijini Dar es Salaam wa mabao 2-1 dhidi ya timu ya KMC umeiwezesha kukwekea hadi nafasi ya pili kibabe kwa kufikisha alama 19 katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Mchezo kati ya timu ya Yanga' Timu ya Wananchi na KMC umefanyika leo katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.Katika mchezo ambao Yanga walikuwa wageni.
Katika mchezo huo ulioanza saa 10 jioni, timu ya KMC ndio walikuwa wakwanza kupata bao lililofungwa dakika ya 27 ya kipindi cha kwanza.Goli hilo lilipachikwa wavuni kupitia mshambuliaji wake mahiri Hassan Kabunda aliyepiga shuti ambalo lilmshinda mlinda mlango wa Yanga Metacha Mnata.
Mashambulizi yaliendelea kwa kila timu kuonesha umaridadi mkubwa wa kusakata soka lenye ufundi lililoambatana na udambwidambwi mwingi.Hata hivyo Yanga walionekana kiwa na kiu ya kutafuta alama tatu muhimu,hivyo waliendeleza mashambuli na ilipofika dakika ya 40 ya mchezo walipata penati baada ya mlinzi wa KMC kumchezea rafu mshambuliaji wa Yanga Michael Sarpong.
Penati hiyo ambayo Yanga waliipata ilipigwa na Tuisila Kisinda na kumfanikisha kufunga baada ya kupiga kwa umaridadi wa hali ya juu na kumfanya mlinda mlango Juma Kaseja akibaki akishuhudia mpira unaingia wavuni.Hivyo hadi wanakwenda mapumziko timu hizo zilikuwa sare ya 1-1.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi na kila timu ikishambulia lango la mwenzake huku Yanga wakionekana kulisakama lango la KMC ambapo mpira wa kona uliopigwa na Farid Mussa aliyetokea benchi akichukua nafasi ya Deus Kaseke mwanzoni tu katika kipindi cha pili ambapo mpira wake wa kona uliyomkuta Waziri Junior ukatosha kuipatia Yanga bao la pili na la ushindi .
Katika mchezo huo KMC walikuwa wakijaribu kujibu mapigo katika dakika za mwishoni za mchezo huo na kushindwa kupata bao la kusawazisha wala la ushindi.Hadi filimbi ya mwamuzi wa mchezo huo Ramadhani Kayoko ilitamatisha mchezo huo kwa Yanga kuibuka na ushindi wa mabao mawili kwa moja dhidi ya KMC.
Mara baada ya mchezo huo Yanga imeendelea kujichimbia katika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi kuu huku wakicheza michezo saba na kupata alama 19 wakati kwa upande wa KMC wakishika nafasi ya sita wakiwa na alama 11. Timu ya Azam ndio inayoongoza kwa kuwa na alama 21 wakati Simba ikishika nafasi ya nne kwa kuwa na alama 13.
0 Comments