Mkuu wa jeshi la polisi nchini Nigeria ameamuru matumizi ya rasilimali zote za polisi ili kumaliza vurugu na vitendo vya uporaji vilivyodumu kwa siku kadhaa.
Wimbi jipya la vitendo vya uporaji liliripotiwa sikuya Jumapili, siku moja baada ya Bw. Adamu kuamuru polisi kukomesha ''vurugu, mauaji, uporaji na uharibifu wa mali''.
Maandamano hayo ya kushinikiza kukoma kwa ukatili wa polisi yalianza tarehe 7 mwezi Oktoba.
Maandamano yalianza tarehe 7 mwezi Oktoba huku vijana wakidai kuvunjwa kwa kikosi cha polisi cha SARS.
Rais Muhammadu Buhari alivunja kitengo cha Sars - kilichokuwa kikituhumiwa kwa unyanyasaji, mateso na mauaji ya kiholela - siku chache baadaye, lakini maandamano hayo yameendelea, yakidai mageuzi makubwa kuhusu namna Nigeria inavyoongozwa.
Maandamano yaloioshika kasi baada ya waandamanaji ambao hawakuwa wamejihami walishambuliwa jijini Lagos siku ya Jumanne. Shirika la Amnesty International lilisema kuwa vikosi vya usalama vimewaua watu karibu 12. Polisi walikana kuhusika na matukio hayo.
Lagos imekumbwa na vitendo vya uvamizi na uporaji kwenye maduka, maduka makubwa mabohari na mali zimeharibiwa siku za hivi karibuni, huku biashara za wanasiasa maarufu zikilengwa.
Majengo kadhaa yamechomwa moto na magereza kushambuliwa.
Siku ya Jumapili, kulikuwa na ripoti za maghala ya serikali kuvamiwa katikati mwa mji wa Jos, na pia katika majimbo ya Adamawa na Taraba, na watu wakichukua chakula na vifaa vya kilimo.
Kulikuwa pia na taarifa kama hizo mjini Bukuru , karibu na mji wa Jos, siku ya Jumamosi.
Maghala hayo yalielezwa kuhifadhiwa chakula kwa ajili ya kuvisambaza wakati wa marufuku ya kutotoka nje iliyowekwa kudhibiti kuenea kwa ugonjwa wa Covid-19.
Rais wa Nigeria Muhammad Buhari amesema watu 69 wameuawa kwenye maandamano na vurugu tangu yalipoanza nchini Nigeria- waliouawa ni raia, lakini pia polisi na wanajeshi.
Siku ya Jumamosi, jeshi la polisi la Nigeria liliandika kwenye ukurasa wa twitter kwamba Bw Adamu, inspekta jenerali wa polisi, alikuwa amewaambia "inatosha" na aliwaamuru maafisa "watumie njia zote halali kusitisha vitendo vya uvunjaji sheria ".
Kundi ambalo limekuwa mbele katika kuratibu maandamano siku ya Ijumaa liliwataka watu kubaki majumbani mwao.
Umoja wa wanaharakati wa wanawake pia umewataka watu kufuata masharti ya muda wa kuwepo majumbani yatakayowekwa kwenye majimbo yao.
Kikundi hicho kilisema hakitachukua tena michango kwa ajili ya maandamano ya #EndSARS.
0 Comments