Freeman Mbowe

Mchakato wa kutangaza matokeo ya washindi wa uchaguzi nchini Tanzania yanaendelea kutangazwa na tume ya uchaguzi nchini Tanzania.

Watanzania wameshuhudia anguko la wapinzani kwenye ngome zao mbalimbali zikinyakuliwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa nafasi za udiwani na ubunge.

Freeman Mbowe

Mwenyekiti wa chama cha upinzani Chadema ambaye pia alikuwa mbunge wa Jimbo la Hai huko Moshi. Freeman Mbowe ameshindwa kutetea kiti chake, baada ya kushindwa kwenye sanduku la kura na mgombea wa CCM, Saashisha Mafuwe.

Saasisha Mafuwe CCM ameongoza kwa kura 89,786 dhidi ya kura 27,684 za Freeman Mbowe.

Freeman Mbowe amekuwa mbunge wa Chadema kwa miaka 10

Zitto Kabwe:

Alikuwa mgombea ubunge wa jimbo la Kigoma mjini kwa tiketi ya ACT-Wazalendo. Zitto amekuwa mbunge kwa miaka 15, miaka 10 jimbo la Kigoma Kaskazini, na miaka mitano jimbo la Kigoma mjini ambalo alikuwa akitetea kiti chake.

Zitto Kabwe

Zitto amebwagwa na mgombea wa CCM Kilumbe Ng'enda. Kwa mujibu wa matokeo rasmi yaliyotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi NEC, Ng'enda amepata kura 27,688 huku Zitto akipata kura 20,600.

Joseph Mbilinyi

Sugu

Joseph Mbilinyi maarufu Mr.Two au Sugu amekuwa mbunge wa Mbeya mjini kupitia chama cha upinzani cha chadema nchini humo tangu mwaka 2010 mpaka 2020.

Mgombea wa Chama cha mapinduzi katika jimbo la Mbeya mjini Dkt. Tulia Akson ameibuka mshindi katika uchaguzi wa eneo hilo.

Dkt Tulia Akson alimshinda Sugu kwa kura 75,225 dhidi ya kura 37,591 za Joseph Mbilinyi.

Joseph Haule:

jay

Msanii wa Bongo Fleva Joseph Haule maarufu Profesa Jay wa chama cha CHADEMA ameshindwa kutetea jimbo la Mikumi, ambalo alikuwa mbunge kwa kipindi cha miaka mitano.

Profesa Jay amepata kura 17,375 huku mpinzani wake Denis Lazaro wa chama cha CCM akiibuka mshindi kwa kupata kura 31,411.

Profesa Jay alipata umaarufu mkubwa kwa kibao chake cha 'ndio mzee'.

Godbless Lema

Godbless Lema wa Chadema ameshindwa kutetea jimbo lake la Arusha mjini baada ya kushindwa na mgombea wa CCM, Mrisho Gamba aliyepata kura 82,480 na huku Lema akiwa na kura 46,489.

Lema amekuwa mbunge kwa kipindi cha miaka 10.