MAMBO vipi mpenzi msomaji wa safu yako pendwa ya My Style? Kama ilivyo kawaida huwa tunakutana hapa na kupiga stori nyingi na mastaa mbalimbali hapa Bongo, ambapo tunapata nafasi ya kujua life style yao kwa ujumla iko vipi.
Leo tupo na aliyekuwa mume wa msanii wa muziki wa Bongo Fleva, Zuwena Mohammed ‘Shilole’, Ashraf Uchebe, ambaye amefunguka mambo mengi usiyoyajua kutoka kwake, ungana nami kwa mahojiano kamili:
My Style: Ratiba yako kwa siku huwa ikoje?
Uchebe: Siku hizi ratiba yangu imebadilika kidogo, huwa naamka alfajiri kisha naenda kuswali, nikitoka hapo naingia gym kwa ajili ya kufanya mazoezi, baada ya hapo ndio naenda ofisini kwangu.
My Style: Mtu wa kwanza kumpigia simu huwa ni nani pindi unapoamka?
Uchebe: Mtu wa kwanza kumpigia simu huwa ni mama yangu mzazi kwa sababu anakaa na mwanangu hivyo lazima nipige simu ili kujua wameamkaje na wanaendeleaje.
My Style: Starehe yako kubwa ni nini?
Uchebe: Starehe yangu kubwa na ya kwanza ni kufanya ibada.
My Style: Jambo gani ambalo umewahi kulifanya huko nyuma kisha baadae ukajutia kwa nini ulilifanya?
Uchebe: Ni vitu vingi sana, kwa sababu kila binadamu ana hasira na mapungufu yake, kwa hiyo ni ngumu sana kukusanya mambo yote, kwa sababu vipo vitu vingi sana ninavyojutia kuvifanya na Mungu naomba aninusuru.
My Style: Umeshawahi kwenda kwa mganga ili kuweka mambo yako sawa?
Uchebe: Hapana, mimi huwa nafanya dua tu, sijawahi kwenda kwa mganga wala nini.
My Style: Ukipewa nafasi ya kurudisha kitu kimoja ambacho umewahi kukipoteza huko nyuma, utatamani kurudisha kitu gani?
Uchebe: Mmmh! Swali gumu sana kwangu hilo.
My Style: Kwa faida ya wasiokujua, ukiwa na hasira unakuwaje?
Uchebe: Ni vigumu sana mtu kunijua, kwa sababu hata dini yangu inasema kuwa ni vyema mtu anapokuwa na hasira asiionyeshe kwa mwenzie, ndio maana mimi hata nikiwa nimekasirika huwa natabasamu, hivyo ni ngumu mtu kujua kama nina hasira au sina.
My Style: Ukiwa na msongo wa mawazo huwa unapenda kufanya vitu gani ili kuiweka hali yako sawa?
Uchebe: Mara nyingi nikiwa na msongo wa mawazo huwa napenda kutulia peke yangu, halafu pia huwa natafakari na kumuomba Mwenyezi Mungu anifanyie wepesi ili vitu vikae sawa.
My Style: Wewe ni mtu wa marafiki sana au sio?
Uchebe: Ndio, napenda sana kuwa na marafiki mbalimbali, kwa sababu ndio inasaidia kujuana na watu wengi na inakufanya uweze kufanya vitu tofautitofauti. Kwa sababu kwenye maisha hakuna mtu anajiendesha mwenyewe, lazima ubadilishane mawazo na wengine ili uweze kufika mbali zaidi.
My Style: Imeshawahi kukutokea mtu akakudharau kutokana na muonekano ulionao kwa sababu ya kazi unayofanya ya ufundi magari?
Uchebe: Kuna mtu sitaki kumtaja jina niliwahi kumpigia simu kipindi hicho ndio naanza kutokatoka, kwa hiyo nikampigia simu kisha nikajitambulisha mimi fulani akanijibu kwa dharau sana, halafu kikapita kama kipindi fulani hivi hali yangu ikabadilika nikawa najulikana sana. Nikaja kukutana naye tena, alivyoniona akaona aibu kweli, niwe mkweli sikumsalimia kwa sababu mimi ni binadamu pia naumia.
My Style: Kwa watu ambao hawakujui wewe ni mtu wa aina gani?
Uchebe: Mimi ni mtu tofauti sana, halafu naishi maisha yangu, maisha ambayo mwenyezi Mungu anataka niishi, pia napenda kuishi na watu vizuri.
0 Comments