JESHI la Polisi Mkoa wa Shinyanga linafanya uchunguzi kuhusiana na tukio la jaribio la kuchoma moto nyumba ya Mbunge Mteule wa Jimbo la Shinyanga Mjini Patrobas Katambi (CCM) iliyopo mtaa wa Ushirika Mjini Shinyanga.

Pia limemkamata aliyekuwa Mgombea Ubunge Jimbo la Shinyanga Mjini kupitia CHADEMA Salome Makamba na mdogo wake Timoth Makamba wakihusishwa na tukio hilo.



Akitoa Taarifa kwa Vyombo vya Habari leo Oktoba 30,2020 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba amesema tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia leo majira ya saa sita na dakika 45.

 “Majira ya saa saba kasorobo, Mbunge Mteule Patrobas Katambi akiwa amelala  nyumbani na ndugu zake walisikia kishindo juu ya paa la choo cha nje ambacho kipo katika eneo la uzio wa nyumba hiyo ndipo walipotoka nje na kuona moto ukiwaka juu ya paa la choo pamoja na dumu lenye mafuta aina ya petroli”,ameeleza Kamanda Magiligimba.

“Wakati  wakiendelea kuzima moto huo waliona gari aina ya Toyota Klugger lenye rangi ya silver likikimbiliwa na watu wawili na kisha watu wale waliingia ndani ya gari lile na kutoweka”,amesema Kamanda Magiligimba.

Kamanda Magiligimba amesema baada ya kufanikiwa kuzima moto huo waliona gari lile lile likipita barabara ya lami ya Shinyanga – Mwanza ndipo walipoamua kulifuatilia na dereva wa gari hilo baada ya kugundua anafuatiliwa aliamua kuingia hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga na kuliacha gari hilo kisha kukimbia.

“Wakati wa kuwaweka chini ya ulinzi watu hao ilitokea purukushani ndani ya uzio wa hospitali na gari ya polisi iliyokuwa doria ilifika mapema na kufanikiwa kuwakamata watu wawili ambao ni Wilson Mhando Suluti (30) mkazi wa Bugweto na Jackson Raphael Peter (27) mkazi wa Bugweto wakiwa ndani gari hilo lenye namba za usajili T 729 DFP aina ya Toyota Klugger rangi ya Silver mali ya Salome Makamba aliyekuwa mgombea ubunge Jimbo la Shinyanga Mjini kupitia CHADEMA”,amefafanua Kamanda Magiligimba.

“Ilibainika kuwa watu hao tuliowakamata wao ndiyo waliokuwa kwenye eneo la tukio kulingana na mavazi waliyovaa. Baada ya mahojiano, watu hao walikiri kuwa gari hilo ni la Salome Makamba na dereva aliyetoroka ni Timoth Makamba ambaye ni mdogo wake Salome Makamba”,ameongeza.

Amesema polisi walifika nyumbani kwa Salome Makamba na kufanya upekuzi kisha kuwakamata watu wengine wawili ambao ni Justine Owesiga (35) Mkazi wa Ndala Shinyanga na Gibson Mkongwa (31) mkazi wa Iringa waliokutwa kwenye nyumba hiyo.

“Juhudi za kuwatafuta na kuwakamata Salome Makamba na Timoth Makamba ambaye ndiye dereva wa gari hilo lililotelekezwa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga zinaendelea. Gari husika linashikiliwa na watuhumiwa hao wanne na watafikishwa mahakamani upelelezi utakapokamilika”,amesema.

Amesema Salome Makamba aliachiwa jana kwa dhamana baada ya kushikiliwa na jeshi la polisi Oktoba 28,2020 kwa tuhuma za kumshambulia msimamizi wa uchaguzi kituo cha kupigia kura cha Bugweto B, Farida John na kumuumiza ambapo aliomba aone matokeo na baada ya kutoridhika nayo aliyachana na kuanza kumshambulia msimamizi huyo wa uchaguzi akiwa na wafuasi wake.