RIPOTI iliyochapishwa na programu ya mazingira ya Umoja wa Mataifa (UNEP), imesema mamilioni ya magari ya mitumba yanayochafua mazingira kutoka nchi tajiri huuzwa katika nchi zinazoendelea, ikiwa ni njia ya kuyatupa.
Kati ya mwaka 2015 na 2018, magari karibu milioni 14 na zaidi, yenye ubora duni yalisafirishwa kutoka Ulaya, Japan na Marekani.
Magari kati ya manne kati ya matano yaliuzwa kwa nchi masikini, huku zaidi ya nusu yakiuzwa Afrika.
Wataalamu wanasema karibu asilimia 80 ya magari hayo yameshindwa kufikia viwango vya chini vya usalama na mazingira katika nchi zinazosafirisha nje.
Pamoja na kusababisha ajali, magari haya hufanya uchafuzi wa hali ya hewa na kuchangia mabadiliko ya tabia nchi.
Ripoti hiyo inasema magari mengi yameharibiwa kwa kuondoa vipuri vya thamani.
Ilisema wasafirishaji na wanunuaji kutoka nje wanapaswa kuweka masharti makali ili kuondokana na hali hiyo.
Umiliki wa gari unakua ulimwenguni kote kukiwa na makadirio ya magari bilioni 1.4 barabarani, idadi ambayo inatarajiwa kufikia bilioni mbili mwaka 2040.
Kiasi cha ukuaji huo uko katika nchi zinazoendelea katika bara la Asia, Afrika na Amerika Kusini.
Katika uchambuzi wao wa miaka mitatu, watafiti wamegundua kuwa sheria kuhusu uingizwaji magari katika nchi 146 ni dhaifu au dhaifu sana.
Utafiti mwingine kuhusu suala hilo, uliofanywa na taasisi ya Human Environment and Transport Inspectorate, ya Uholanzi unaonesha magari mengi yaliyosafirishwa kutoka bandari za Uholanzi kwenda Afrika yamekwisha muda wake na kuchangia uchafuzi wa hali ya hewa katika bara hilo.
”Tunachoweza kusema ni kuwa kati ya magari milioni 14 karibu asilimia 80 hayafai kuwa barabarani na hayakidhi viwango vya mwisho vinavyotakiwa viitwavyo Euro 4,” alisema Rob de Jong, kutoka Unep, mmoja kai ya waandishi wa ripoti.
Viwango vya magari vya Euro 4 vilianza kutumika Ulaya Januari mwaka 2005.
“Hiyo inamaanisha magari hayo hutoa uzalishaji wa hewa chafu zaidi ya asilimia 90 kwa sababu hayafikii kiwango hiki kidogo,” alisema de Jong.
Kwa mujibu wa waandishi wa ripoti, magari haya ni ”hatari na machafu.”
Wanaamini uingizwaji wa magari haya yasivyo na ubora unasababisha ongezeko la ajali za barabarani katika nchi nyingi za Afrika na Asia. Magari haya hutoa hewa ambayo huwa chanzo cha uchafuzi wa hali ya hewa kwa kiasi kikubwa katika miji mingi.
”Mwaka 2017, kwa wastani umri wa gari inayotumia dizeli iliyoingizwa Uganda ni zaidi ya miaka 20,” alisema Jane Akumu, wa Unep.
”Hadithi ni hiyo hiyo kwa Zimbabwe, karibu nchi 30 za Afrika hazina umri maalumu kwa magari, hivyo gari la aina yoyote lenye umri wowote, linaweza kuingia.”
Pamoja na kutofikia viwango vya usalama barabarani na mazingira, idadi kubwa ya magari vifaa muhimu viliondolewa.
“Walikata, vifaa kama catalytic converters kwa sababu thamani ya platinamu ni dola 500. Na waliweka kipande cha bomba la chuma na kuiunganisha,” alisema Rob de Jong.
“Wameondoa mifuko ya hewa kinyume cha sheria, kwa sababu ina thamani huko Ulaya, wameondoa kinyume cha sheria mfumo wa kuzuia breki kwa sababu una thamani na huuzwa kwenye soko la magendo.”
Kati ya magari yaliyoelezwa kwenye ripoti hiyo, zaidi ya asilimia 54 yalitoka Ulaya. Mengi yalisafirishwa kupitia Uholanzi.
Mamlaka za Uholanzi zimeonesha wasiwasi kuhusu biashara hiyo na zimetaka hatua zichukuliwe kwenye ngazi ya Umoja wa Ulaya
”Uholanzi haiwezi kushughulikia suala hili peke ,” alisema Stientje van Veldhoven, Waziri wa Mazingira wa Uholanzi alisema.
“Kwa hivyo, nitatoa wito kwa Ulaya kushirikiana na serikali za Afrika, kuhakikisha nchi za EU zinasafirisha magari ambayo yako katika viwango vinavyotakiwa kwa ajili ya matumizi vilivyowekwa na nchi zinazosafirisha.”
Kutokana na kutambua hatari inayoletwa namagari haya, nchi kadhaa zimekuwa zikifanya sheria kuwa madhubuti zaidi.
Morocco inaruhusu magari yaliyo na umri wa chini ya miaka mitano kuingizwa nchini humo. Kenya ni magari yasiyozidi miaka minane.
Katika ngazi za kikanda, Jumuia ya Kiuchumi ya nchi za Magharibi mwa Afrika, ECOWAS, yenye wanachama 15, imeweke viwango kwa mafuta na magari kuanzia mwezi Januari mwaka 2021.
Lakini kukabiliana na suala hili kunahitaji hatua kuchuliwa na pande zote mbili katika mnyororo wa kibiashara.
”Kwa upande mmoja, ni kinyume cha maadili kuwa nchi zilizoendelea zinasafirisha kwenye barabara zao wenyewe magari ambayo hayana viwango vya kuwa barabarani ,” alisema Rob de Jong.
“Kwa upande mwingine, kwa nini nchi zinazoingiza magari zimekuwa zikisubiri kwa muda mrefu kuweka viwango vya chini?
“Kwa hivyo nadhani jukumu sio tu kwa nchi inayouza nje, kwa kweli ni jukumu la pamoja.”
0 Comments