KASHMIR, INDIA

MADUKA na sehemu zote za biashara zimekufungwa leo katika jimbo la Kashmir, na wakazi wengi walibakia majumbani baada ya vikundi vya kisiasa na vya kidini kuitisha mgomo wa kuipinga sheria mpya inayowaruhusu watu wa nje kununua ardhi katika eneo hilo lenye mgogoro.

Vikosi vya ziada vya usalama vya India vilivyotumwa katika eneo hilo, vilifanya doria katika barabara zilizokuwa tupu.

 Hayo yametokea baada ya mapema wiki hii serikali ya India kutangaza kuondoa sheria ambazo zilikuwa zinahakikisha ni wakazi wakudumu pekee wanaoweza kumiliki ardhi katika eneo hilo. Ni mgomo mkubwa kushuhudiwa tangu Waziri Mkuu wa India Narendra Modi kuyabatilisha mamlaka ya utawala wa ndani ya upande wa Kashmir unaosimamiwa na India.

Wakati huo huo  Nchi za Ulaya zimesema Shirika la Afya Ulimwenguni WHO linastahili kuwa na nguvu ya kuchunguza kwa uhuru milipuko ya magonjwa na pia kuweza kuzilazimisha nchi kutoa data zaidi. 

Wito huo umetolewa baada ya kutokea janga kubwa la virusi vya corona ambalo limewezesha kuonyesha mapungufu katika shirika hilo. 

Waziri wa afya wa Ujerumani Jens Spahn amesema WHO inapaswa kuungwa mkono zaidi kisiasa na kifedha kutokana na juhudi zake za kusimamia migogoro ya kiafya. 

Nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya zimetoa mapendekezo kadhaa ya kulirekebisha shirika hilo la afya duniani. Wakati huo huo mkurugenzi mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema wataalam wa Shirika hilo walilijadili janga la corona hapo jana katika mkutano na wenzao wa China.