Viongozi wa upinzani Tanzania

Vyama vikuu vya upinzani nchini Tanzania Chadema na ACT-Wazalendo vinataka kurejewa kwa Uchaguzi Mkuu nchini humo.

Vyama hivyo viwili vinapinga matokeo ya uchaguzi wa Jumatano ambapo rais aliye madarakani John Magufuli amekwishatangazwa mshindi.

Katika mkutano wa wanahabari wa pamoja baina ya viongozi wa Chadema na ACT Wazalendo vyama hivyo pia vimeitisha maandamano ya nchi nzima ili kudai kurejewa kwa uchaguzi huo.

Mwenyekitiwa Chadema Taifa Freeman Mbowe ameeleza kuwa: ''kilochofanyika si uchaguzi ni unyang'anyi wa demokrasia uliofanywa na ZEC (Tume ya Uchaguzi Zanzibar) na NEC (Tume ya Taifa ya Uchaguzi) .''

Freeman Mbowe
Maelezo ya picha,

Mwenyekitiwa Chadema Taifa Freeman Mbowe

Vyama hivyo sasa vinataka kuvunjwa kwa Tume ya NEC na ZEC.

Vyama hivyo aidha vimewaomba Watanzania kufanya maandamano ya amani.

''Kuanzia Jumatatu, wanachama wa vyama vyetu na wote wasiokubaliana kushiriki katika maandamano ya amani kuanzia Novemba 2 hadi hapo madai yetu yakapotelekezwa'' walisema.

Siku ya Alhamisi Mwenyekiti wa ACT Wazalendo ambaye pia alikuwa mgombea wa urais visiwani Zanzibar, Maalim Seif Seif Sharif Hamad alikamatwa pamoja na viongozi wengine wa chama hicho.

Kamanda wa Polisi Mjini Magharibi Zanzibar Awadhi Juma alisema Maalim Seif alikamatwa akiwa anafanya maandamano ambayo hayana kibali akiwa na wafuasi wa chama chake.

Maelezo ya video,

Matokeo ya Uchaguzi Tanzania: Kwanini tulimkamata Maalim Seif?

Siku ya Alhamisi Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania ulizitaka mamlaka za taifa hilo la Afrika Mashariki kushirikiana na wadau mbalimbali kushughulikia kwa uwazi malalamiko yanayotolewa kuhusu uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 28 mwaka huu.

Ubalozi huyo kupitia tamko lake lililotolewa Oktoba 29, mwaka huu unasema kufanya hivyo kutarejesha imani na kutekeleza azma ya kuheshimu utawala wa sheria na dhana ya utawala bora.

Moja ya malalamiko yaliyotajwa na ubalozi huo ni kuhusu uwepo wa kura feki katika uchaguzi huo.

NEC imesemaje?

Malalamiko hayo yalishatolewa ufafanuzi na kupingwa na Tume ya taifa ya uchaguzi kwamba hayana ukweli kupitia kwa mwenyekiti wake, Jaji Kaijage.

''Kuna taarifa zinazosambaa katika mitandao ya kijamii kuhusu kuwepo kwa masanduku ya kura feki katika majimbo ya Kawe Dar es Salaam, Pangani Tanga na Buhigwe Kigoma", alisema Bw. Kaijage.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi imesema haijapokea taarifa ya madai hayo.