BAADA ya Yanga kufanikiwa kutwaa ubingwa wa Kombe la Mapinduzi kwa kuifunga Simba kwa mikwaju ya penalti 4-3, imebainika kuwa uongozi wa timu hiyo umetoa kitita kisichopungua milioni 300 kwa benchi la ufundi la timu hiyo pamoja na wachezaji.
Katika fainali hiyo ya Mapinduzi iliyofanyika Jumatano iliyopita kwenye Uwanja wa Amaan visiwani Zanzibar, ilishuhudiwa na mabosi wote wa Yanga wakiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa GSM ambao ni wadhamini wa Yanga, Ghalib Said Mohamed, Mkurugenzi Mtendaji wa GSM Eng.Hersi Said, Mwenyekiti Mkuu wa Yanga, Dk Mshindo Msolla na Mshauri Mkuu wa Mabadiliko wa timu hiyo, Senzo Mbatha Mazingisa ambao walifurahishwa na ubingwa huo.
Chanzo chetu cha kuaminika ndani ya Yanga kililiambia Championi Jumamosi kuwa, hapo awali kabla ya mchezo kufanyika mabosi waliongea na Yanga kwa zaidi ya saa moja na nusu ambapo mwishoni waliweka ahadi ya milioni 200 kama wangeweza kutwaa kombe hilo lakini baada ya kufanikiwa kutwaa waliongeza na kufikia mil 300.“Baada ya Yanga tu kutinga hatua ya fainali na wakajua kuwa wanaenda kucheza dhidi ya Simba katika fainali hiyo viongozi wa Yanga walikaa na wachezaji na kuzungumza kwa zaidi ya saa moja na nusu, kikubwa walikuwa wakizungumza ni namna gani wataweza kuutwaa ubingwa huo.
“Hivyo kupitia kikao hicho mabosi wa Yanga waliahidi kiasi cha milioni 200 kwa wachezaji wa Yanga ili kuwaongezea ari ya kupambana kuhakikisha kuwa wanabeba kombe mbele ya watani wao Simba.“Cha ajabu baada ya kufanikiwa kutwaa kombe hilo kwa changamoto za mikwaju ya penalti 4-3, viongozi na mabosi wa Yanga wakaongeza kiasi cha fedha kutoka milioni 200 mpaka kufikia milioni 300 na kupelekea furaha kubwa kwa wachezaji na benchi la ufundi ambalo limeahidi kuutwaa na ubingwa wa ligi kuu,” alisema mtoa taarifa huyo.
Wachezaji wa Yanga walioahidi ubingwa kupitia Championi Jumamosi ni Paul Godfrey Boxer ambaye alisema kuwa licha ya kutwaa taji hilo nguvu zao kwa sasa wanazihamishia katika ubingwa wa ligi kuu.“
Tayari tumeshamaliza kazi yetu ambayo tulikuja kuifanya huku visiwani Zanzibar hivyo tunahamishia nguvu zetu kwenye lengo letu kubwa la mwaka huu kuhakikisha kuwa tunatwaa ubingwa wa ligi kuu.
”Naye Abdallah Shaibu ‘Ninja’ alisema kuwa: “Tunamshukuru Mungu kwa kufanikiwa katika hili, haikuwa kazi nyepesi kwetu kufanikiwa ila naamini tumestahili kubeba Kombe la Mapinduzi kwa kuwa tumepambana hivyo mapambano haya tutayahamishia katika ligi kuu ili tuweze kubeba taji la ligi kuu.
0 Comments