IBRAHIM Ame, beki wa kati wa timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars amesema kuwa wanaamini watafanya kweli kwenye michuano ya Chan 2021 inayofanyika nchini Cameroon.
Nyota huyo ambaye mchezo wake wa kwanza ndani ya Stars inayonolewa na Etienne Ndayiragije ulikuwa dhidi ya DR Congo, uliochezwa Uwanja wa Mkapa ulikamilika kwa sare ya kufungana bao 1-1.
Akizungumza na Championi Jumamosi, Ame alisema kuwa kazi kubwa iliyopo kwa wachezaji wote ni kuweza kufanya vizuri kwenye mechi zao zote ambazo watacheza ndani ya uwanja.
“Tunajua kwamba tuna kazi kubwa ya kufanya, tupo tayari kwa ajili ya mashindano ya Chan na wachezaji wote tumekubaliana kufanya vizuri ndani ya uwanja, mashabiki waendelee kutuombea,” alisema Ame ambaye ni beki wa Simba.
Stars ipo Kundi D ikiwa pamoja na timu za Guinea, Namibia na Zambia tayari imeshawasili nchini Cameroon kwa ajili ya mashindano hayo makubwa yanayoshirikisha wachezaji wa ndani. Januari 19, Stars itakuwa kazini ikisaka ushindi dhidi ya Zambia mchezo utakaochezwa saa 1:00 usiku.
STORI: LUNYAMADZO MLYUKA, Dar es salaam
0 Comments