Rais wa Ethiopia Bi. Sahle-Work Zewde

WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba Kabudi amesema kuwa kesho Januari, 25 Tanzania inatarajia kupokea ugeni wa Rais wa Ethiopia Bi. Sahle-Work Zewde kwa ziara ya kikazi ya siku moja Wilayani Chato mkoani Geita.

 

Prof. Kabudi ameyasema hayo leo Januari 24 huko Chato wakati akizungumza na wanahabari kuhusu ujio huo wa rais wa Ethiopia ambapo amesema kuwa mahusiano ya Tanzania na Ethiopia yamekuwa ya shida na raha.

Uhusiano wetu na Ethiopia umekuwa katika hali zote na ni mahusiano ambayo yalitengenezwa na waasisi wa mataifa haya mawili ambayo yamekuwa na manufaa kibiashara,” amesema Prof. Kabudi.

 

Mhe. Sahle-Work Zewde ni rais wa kwanza mwanamke nchini Ethiopia.

 

“Nitumie fursa hii kutoa muhtasari wa uhusiano na ushirikiano kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Ethiopia, Tanzania na Ethiopia zimekuwa na mahusiano ya muda mrefu na ushirikiano mzuri kwa muda wote huo, na uhusiano huu unatokana na msingi mzuri uliojengwa na muasisi wa Taifa letu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere,” amesema Profesa Kabudi.

Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel amewaomba Wakazi wa mkoa huo kujitokeza kwa wingi kumpokea mgeni huyo kama ilivyo desturi yao.

“Niwaombe wana Geita tujitokeze kwa wingi kuanzia majira ya saa 12, tuweze kumpokea mgeni ambaye atakuja katika mkoa wetu wa Geita, mgeni huyo ni Rais wa Ethiopia ambaye majira ya saa nne asubuhi atakuwa ameshawasili,” amesema Mhandisi Gabriel.