Ni takriban wiki moja tangu Taasisi ya tuzo ya Nobel ya Uswidi ilipotangaza kwamba mshindi wa tuzo hiyo kwa upande wa fasihi 2021 ni Abdulrazak Gurnah mwenye umri wa miaka 73.

Gurnah ambaye ni profesa wa Kiingereza aliyestaafu hivi karibuni katika Chuo Kikuu cha Kent Uingereza, ni mzaliwa wa Zanzibar anaishi katika mji wa Cantebury Kusini mashariki ya England, alikowasili 1968. Ushindi wa Gurnah ulipokelewa kwa mchanganyiko wa furaha na mshangao wa wengi kwani huenda akijulikana zaidi Ulaya lakini si kwao alikozaliwa.

Tukio hilo limeibua mjadala mzito sio tu ule wa kwamba mwandishi ni Mzanzibari au Mtanzania, lakini jengine kubwa ni mjadala kuhusu kuporomoka kwa utamaduni wa kusoma vitabu na uandishi fasihi, pakitiliwa mkazo juu ya haja ya kutafakari ili kuondokana na hali hii.

Kuna sababu tofauti zinazotolewa juu ya kuzuka hali hii na kuendelea kupungua au kutoweka utamaduni wa kusoma vitabu, kinyume na ilivyokuwa miaka 40 iliopita na nyuma ya hapo.

Kubadilika badilika kwa mitaala ya elimu ni sababu moja. Mabadiliko hayo yamekuwa na athari kwa mfano katika utaratibu wa elimu likiwemo somo la fasihi. Somo hilo limekuwa likipotea taratibu au kutopewa uzito, kutokana na uchache wa vitabu na waalimu mahiri waliobobea iwe kwa lugha ya Kiswahili au Kiingereza .

Tulikotoka na mfumo uliowekwa kando

Ninakumbuka wakati nikiwa mwanafunzi wa shule ya msingi na sekondari miaka ya 1960 na 70, fasihi iwe kwa lugha ya Kiswahili au Kiingereza, lilikuwa ni somo moja muhimu. Kilichosaidia zaidi ni shauku ya wanafunzi iliotokana na upatikanaji wa vitabu kwa urahisi, kando na mtindo wa kubadilishana.

Ninakumbuka vitabu vya mwandishi Muingereza kama James Hadley Chase. Pamoja na vitabu mbali mbali vya shule kulikuwa na utamaduni wa sisi wenyewe kuazimana sio tu vitabu vya riwaya lakini hata magazeti. Kitu cha kwanza asubuhi mwishoni mwa juma ilikuwa ni hamu ya kusoma magazeti, iwe ni Standard au Nationalist, Mfanyakazi, Ngurumo au Taifa leo na Baraza la Kenya.

Kwa upande wa Kiingereza ni vya mwandishi Shakespear kama " Merchant of Venice," au kitabu maarufu cha mwandishi mahiri wa Kinigeria Chinua Achebe ," Things Fall Apart." Miongoni mwa michezo ya kuigiza ulikuwa ule wa "Romeo and Julliet."

Vitabu vya Abdulrazak Gurnah

CHANZO CHA PICHA,GETTY IMAGES

Ingawa vitabu vya Kiingereza ni vile tulivyorithi kwa wakoloni, kulikuweko na vitabu vya waandishi maarufu wa Kiswahili kama Shaaban Robert na Mathias Myampala au vitabu vya Mohamed Said Abdullah kutoka Zanzibar maarufu Bwana Msa kikiwemo kile cha " Kisima cha Giningi." Wote walikuwa pia mabingwa wa lugha ya Kiswahili.

Kuvurugika kwa mitaala ya elimu na kutokuwa na uhakika wa kilichobora kulitokana pia na kuingizwa siasa katika elimu. Somo la siasa lilipewa kipa umbele. Kwa Tanzania mfumo wa chama kimoja ulichangia mno katika hilo na kuathiri ubora wa elimu hasa kwa kuwa shule zilimilikiwa na serikali na kwa miaka mingi kulikuwa na shule chache za binafsi.

Kwa mujibu wa Mwalimu wa Kiswahili katika Chuo cha Masomo ya Kiorientali na Kiafrika mjini London (SOAS), matokeo yake sasa licha ya watu kusoma magazeti lakini zaidi ni siasa na michezo

Kwa mtazamo huo walionufaika kupata nafasi ya elimu bora ni wale ambao wazee wao waliweza kuwapeleka shule za binafsi. Huko walau mitaala ilikuwa tafauti kukiwemo na somo la fasihi. Kuanguka kwa utamaduni wa kusoma vitabu na fasihi kumechangiwa pia na tija na masilahi duni kwa waalimu ikiwemo mishahara, jambo ambalo limeshusha mori wa kuwajibika ipasavyo.

Maktaba zimesahaulika na athari ya Teknolojia

Kuna hoja ya wakosoaji kwamba Wizara ya elimu haitilii umuhimu kuwepo kwa maktaba na vitabu vya kutosha. Hata maktaba zilizoko mashuleni hazikidhi mazingira yalioko leo kwa maana ya kwenda na wakati.

Hizo ni sababu chache kati ya nyingi. Lakini katika miaka hii ya karibuni, teknolojia ni athari nyengine yenye uzito mkubwa. Wakati matatizo ya ukosefu wa elimu bora katika shule za serikali yakiwa pale pale, wenye uwezo wanaweza kusoma wakitakacho kupitia mitandao na matumizi ya intaneti kwa kiasi wakitakacho.

Licha ya hayo, tafiti mbalimali zinaonesha mitandao ya jamii imewavutia zaidi vijana kugeukia mambo mengine, kuliko kusoma masuala ya kuwaendeleza kielimu. Magazeti ya kile kinachoitwa udaku mitandaoni, ni kivutio kikubwa. Wapo wanaoitumia mitandao na teknolojia ya intaneti kujiendeleza kielimu lakini watafiti wanasema idadi yao ni ndogo.

Hatari kubwa ni kwamba mkondo huo unatishia kuwepo tabaka la waliosoma na kufuzu ambao ndio wanakuwa na urahisi wa kupata ajira au kujiendeleza kimaisha lakini wanashindwa kupiga hatua kielimu. Matokeo yake wasiokuwa na nafasi hizo ambao idadi yao ni kubwa hukumbwa na tatizo la ukosefu wa ajira na kutojua mustakbali wao utakuwaje.

Kiswahili au Kiingereza bado ni mabishano

Baadhi ya wataalamu wanahisi bado ni tatizo kukitumia Kiswahili katika ulimwengu huu ambao lugha za kiingereza na kwa sehemu Kifaransa zimetamalaki. Elimu kwa lugha nyengine iwe Kichina, Kirusi au Kijapani kama inavyodaiwa, haisaidii bila ya kukifahamu kiingereza ingawa inategemea ni fani au taaluma gani. Lugha hizo zina utajiri mkubwa uliojengeka karne nyingi.

Hamza Zubeir Rijal mwanasanyasi mtaalamu wa Mazingira na mhadhiri huru wa Chuo Kikuu cha Zanzibar anasema" Kiswahili kinaweza kuwa lugha ya kusomeshea ikiwa Jumuiya ya Afrika mashariki italibeba hilo kwa pamoja . Patahitajika tafsiri ya vitabu muhimu na kupanga mkakati kwa kipindi cha kuanzia miaka 10 na kuendelea pamoja na kuwa na waalimu wa kutosha waliobobea katika lugha ya Kiswahili."

Huenda Rijal yuko sahihi, kwani kuvunjika Baraza la Kiswahili la Afrika mashariki kumechangia mno kuzorota kwa lugha hii katika kila nchi kwa maana ya Tanzania na Kenya kunakozungumzwa lugha hiyo zaidi, kwenda njia yake yenyewe. Matokeo ni mchafuko wa lugha.

Hoja ya Rijali inaungwa mkono na mwalimu Hadjivayanis, kwamba ni wazi Kiingereza ilikuwa lugha ya Kikoloni, kama Kifaransa na Kireno.Lakini sasa tukubali Kiingereza ni lugha ya dunia , muhimu kifundishwe inavyopaswa.

Kuhusu Kiswahili kuwa lugha ya Kisomeshea ni muhimu kwa wanafunzi kusomeshwa kwa lugha wanayoifahamu ili waweze kuelewa lakini lazima kuweko na uwekezaji wa maana na uhakika, lakini hadi wakati huo Kiingereza kinabaki lugha ya kiulimwengu,anasisitiza Hadjivayanis.

Ushindi wa Abdulrazak Gurnah wa tuzo ya Nobeli katika fasihi, uliandamwa na mjadala anatoka wapi, Zanzibar au Tanzania. Alizaliwa 1948 wakati Tanzania haipo, Lakini binafsi amemaliza ubishi huo katika mahojiano na kipindi cha Focus cha BBC aliposema, ushindi wake ni heshima Kwa Zanzibar, Tanzania na Afrika.

Lakini kwa upande wa mjadala wa kushuka kwa kiwango cha elimu na kupotea utamaduni wa kusoma vitabu, huo bila shaka utaendelea kwa muda na kuna haja na umuhimu wa mfumo wa elimu Tanzania kuangaliwa upya.