RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza Dk.Hussein Mwinyi amewakaribisha wawekezaji pamoja na kampuni mbalimbali kuwekeza Zanzibar huku akiwahakikishia mazingira bora kuhusu uwekezaji wao.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdula ameleza hayo kupitia hotuba aliyoisoma kwa niaba ya Rais Dk. Hussein Mwinyi katika maonesho yaliyoandaliwa na Wizara ya Aridh na maenedeleo ya Makaazi yaliofanyika katika viwanja vya Verde Mtoni.
Ameziomba taasisi za kifedha pamoja na wadau wengine kuchangamkia fursa ya kujenga nyumba za makaazi na kuondosha hofu juu ya uwekezaji huo kutokana na uhitaji mkubwa wa wananchi katika suala la makaazi.
“Nawaomba wawekezaji ondoseheni hofu na wala musiwe na wasi wasi kwani uhitaji wa nyumba Zanzibar ni mkubwa,"amesema Makamu wa Pili wa Rais na kuongeza kuwa Serikali ya awamu ya nane inaendela na mchakato wa kuipanga Zanzibar kwa kuanzisha miji mipya.
"Itakayojengwa nyumba za kisasa ikiwemo Matamwe, Chumbuni na Kilimani kwa upande wa Unguja na kwa upande wa Kisiwani Pemba serikali imetenga maeneo ya Finya na Mfikiwa kwa ajili ya kuanzisha miji mipya.
Ameongeza katika suala la uwekezaji Makamu wa Pili wa Rais amesema Serikali kupitia Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi tayari imetayarisha eneo la Dunga na Pangatupu kama maeneo maalum ya uwekezaji kwa ajili ya ujenzi wa viwanda.
Amebainisha kuwa, Zanzibar ikiwa nchi ya visiwa ina eneo dogo kijografia hivyo, amewaelekeza wataalamu wa Wizara ya Aridh na maendeleo ya Makaazi kuendelea kuipanda ardhi yake kwa kuzingatia sera ya mipango miji.
Katika hatua nyengine Makamu wa Pili wa Rais amewapngeza wizara ya Ardhi na maendeleo ya makaazi kwa ubunifu wao katika kufanikisha maonesho hayo muhimu na ameuzagiza uongozi wa Wizara hiyo kuyaendeleza maonesho kila mwaka.
Pamoja na mambo mengine Hemed amewataka masheha kutoa ushirikiano kwa kusimamia suala zima la mipango miji katika maeneo yao ili kuepuka ujenzi holela.
Kwa upande Waziri wa Ardhi na maendeleo ya Makaazi Mhe. Rizi Pembe Juma amemueleza Mkamu wa Pili Wa Rais wa Zanzibar kwamba kufanyika kwa maonesho hayo kunalenga kuunga mkono dhana ya uchumi wa Buluu ambayo inadhamiria kuinua hali ya uchumi wa Zanzibar pamoja na hali za wananchi wake.
Pia ameeleza maonesho hayo yatatoa fursa kwa wafanyabiashara pamoja na wadau wengine kukutana pamoja na kubadilishana uzoefu juu ya masuala ya makaazi.
Ametoa mwito kwa wadau hao pamoja na wananchi kwa ujumla kuzitumia vizuri siku tatu za maonesho hayo kwa kujifunza mambo mbali mbali yanayohusiana na masuala ya makaazi.
Akitoa maelezo ya Kitaalmu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Joseph Kilangi amesema kutokana na ongezeko kubwa la watu limesababisha wizara kuja na mpango madhubuti kwa ajili ya matumizi bora ya ardhi kwa kuipima na kuipanga ardhi sambamba na kujenga nyumba za gharama nafuu.
Kauli mbiu ya maonesho hayo inasema “Matumizi bora ya ardhi ni fursa ya kukuza uchumi wa Zanzibar."
Kwa upande wake Meneja Uhusiano wa NCBA, Mulindwa Tishekwa amesema wote wanafahamu kuwa nyumba ni ndoto ya watu wengi katika safari ya maisha yao, hivyo mipango mingi katika maisha huenda sawa endapo mtu anakuwa na makazi bora na ya kudumu yanayokidhi mahitaji ya familia.
“Katika maonesho haya NCBA tumekuja kuwapatia habari njema wateja na washiriki wote kwamba tunazo huduma ambazo zinaweza kupelekea ndoto zao kukamilika. Mikopo yetu nafuu itakayowawezesha kujenga au kukamilisha nyumba na ujenzi wa aina yoyote kwa watu binafsi, makampuni na mashirika,” amesema Tishekwa.
Uamuzi wa NCBA kujikita zaidi katika utoaji wa elimu ya kutosha kwa washiriki wote katika maonyesho haya ni kwasababu tumegundua kuwa tunazo bidhaa na huduma nzuri zinazofaa sekta hii lakini wateja wengi hawazichangamkii katika kurahisisha shughuli za ujenzi wa nyumba na miradi mbalimbali.
Ujenzi wa aina yoyote ile unahitaji maamuzi sahihi ambayo yanawezeshwa na taarifa za kutosha ikiwemo namna bora ya kupata usaidizi wa kifedha ili kukamilisha ulichokikusudia.
0 Comments