Wadau waliohudhuria katika maonesho yaliondaliwa na Wizara ya Ardhi na maendeleo ya Makaazi wakimueleza Makamu wa wa Pili wa Rais wa Zanzibar bidhaa mbali mbali wanazodhalisha pamoja na huduma wanazozitoa wakati Makamu wa Pili akiyakagua mabanda katika maonesho hayo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na watendaji wa serikali pamoja wananchi waliohudhuria katika maonesho yalioandaliwa na Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya makaazi yaliofanyika katika viwanja vya Verde ambapo Mhe. Hemed alimuwakilisha Rais Dk. Mwinyi.
Waziri wa Aridhi na Maendeleo ya makaazi Mhe. Riziki Pembe Juma akimueleza Mhe. Hemed hatua zinazochukuliwa na Wizara yake katika katika kuwavutia wawekezaji kuja kuekeza Zanzibar katika masuala ya maakazi katika shughuli ya maonesho yaliofanyika katika Viwanja vya Verde Mtoni.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza amewakaribisha wawekezaji pamoja na Makampuni mbalimbali kuja kuwekeza Zanzibar huku akiwahakikishia mazingira bora juu ya uwekezaji wao.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdula ameleza hayo kupitia hotuba aliyoisoma kwa niaba ya Rais Dk. Mwinyi katika maonesho yalioandaliwa na Wizara ya Aridh na maenedeleo ya Makaazi yaliofanyika katika viwanja vya Verde Mtoni.
Alizishajihisha taasisi za kifedha pamoja na wadau wengine kuchangamkia fursa ya kujenga nyumba za makaazi na kuondoa hofu juu ya uwekezaji huo kutokana na uhitaji mkubwa wa wananchi katika suala la makaazi.
“Nawaomba wawekezaji ondoseheni hofu na wala musiwe na wasi wasi kwani uhitaji wa nyumba Zanzibar ni mkubwa” Alisema Makamu wa Pili wa Rais
Mhe. Hemed alieleza kuwa serikali ya awamu ya nane inaendela na mchakato wa kuipanga Zanzibar kwa kuanzisha miji mipya itakayojengwa nyumba za kisasa ikiwemo Matamwe, Chumbuni na Kilimani kwa upande wa Unguja na kwa upande wa Kisiwani Pemba serikali imetenga maeneo ya Finya na Mfikiwa kwa ajili ya kuanzisha miji mipya.
Aidha, Katika suala la uwekezaji Makamu wa Pili wa Rais alisema serikali kupitia Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi tayari imetaarisha eneo la Dunga na Pangatupu kama maeneo maalum ya uwekezaji kwa ajili ya ujenzi wa viwanda.
Amebainisha kuwa, Zanzibar ikiwa nchi ya visiwa ina eneo dogo kijografia hivyo, amewaelekeza wataalamu wa Wizara ya Aridh na maendeleo ya Makaazi kuendelea kuipanda aridh yake kwa kuzingatia sera ya mipango miji.
Katika hatua nyengine Makamu wa Pili wa Rais amewapongeza wizara ya Ardhi na maendeleo ya makaazi kwa ubunifu wao katika kufanikisha maonesho hayo muhimu na ameuzagiza uongozi wa Wizara hiyo kuyaendeleza maonesho kila mwaka.
Pamoja na mambo mengine Mhe. Hemed amewataka masheha kutoa ushirikiano kwa kusimamia suala zima la mipango miji katika maeneo yao ili kuepuka ujenzi holela.
Nae Waziri wa Ardhi na maendeleo ya Makaazi Mhe. Riziki Pembe Juma amemueleza Mkamu wa Pili Wa Rais wa Zanzibar kwamba kufanyika kwa maonesho hayo kunalenga kuunga mkono dhana ya uchumi wa Buluu ambayo inadhamiria kuinua hali ya uchumi wa Zanzibar pamoja na hali za wananchi wake.
Pia ameeleza maonesho hayo yatatoa fursa kwa wafanyabiashara pamoja na wadau wengine kukutana pamoja na kubadilishana uzoefu juu ya masuala ya makaazi.
Mhe. Riziki alitoa wito kwa wadau hao pamoja na wananchi kwa ujumla kuzitumia vizuri siku tatu za maonesho hayo kwa kujifunza mambo mbali mbali yanayohusiana na masuala ya makaazi.
Akitoa maelezo ya Kitaalmu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Ndugu Joseph Kilangi alisema kutokana na ongezeko kubwa la watu limesababisha wizara kuja na mpango madhubuti kwa ajili ya matumizi bora ya Aridh kwa kuipima na kuipanga aridh sambamba na kujenga nyumba za gharama nafuu.
Kauli mbiu ya maonesho hayo inasema “MATUMIZI BORA YA ARDHI NI FURSA YA KUKUZA UCHUMI WA ZANZIBAR”
Mapema asubhi Makamu wa Pili wa Rais alifika shangani katika eneo la Hotel ya African House kukagua eneo lililoathiriwa na maji ya bahari ambapo alimuagiza Waziri wa Utalii na mambo ya kale kukamisha mchakato Wa muwekezaji ili ujenzi wa eneo hilo uanze mara moja.
0 Comments