Wizara ya afya nchini Tanzania imefunga mashine nyingine kubwa na ya kisasa kwa ajili ya kupima kipimo cha haraka cha UVIKO-19 kwa wasafiri wanaoenda nchi za Falme za Kiarabu ikiwemo Dubai.
Hatua hiyo imekuja kufuatia tangazo la Falme za Kiarabu kutaka wasafiri wanaotokea Tanzania kwenda Dubai, kupata vipimo vya masaa 48 na kisha kumalizia na kipimo cha saa sita kabla ya safari.
Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Aifello Sichalwe amesema kuwa Tanzania ni moja kati ya nchi 6 za Afrika Mashariki ambayo maabara zake zimefanyiwa utambuzi na kukubalika na jumuiya hiyo.
"Nimefika hapa uwanja wa ndege kujionea hali halisi na hali ni nzuri, mashine za kutosha zipo na timu inaendelea na kazi na pia nimeshuhudia eneo la tenti nje ya uwanja ambapo wateja watakapokuwa wanaanzia kupatiwa huduma. Kikubwa wafike mapema na kwa wakati kulingana na muda wa safari zao." alisema Mganga Mkuu Dkt. Sichalwe.
Kwa upande wake, Meneja wa huduma za afya mipakani, ambaye pia ni msimamizi mkuu wa huduma za afya katika uwanja wa ndege wa Julius Nyerere Dar es Salaam, Bw. Remidius Kakuru alieleza kuwa, Wizara imeendelea kupima wasafiri wanaoingia na wanaotoka nchini na zoezi linaenda vizuri.
"Niwasisitize wasafiri kuwa, huduma imeanza kutolewa tokea tarehe 16 mwezi huu na tayari tunaendelea na upimaji kwa wasafiri wanaokwenda Dubai.
Tunawasisitizia wasafiri wajitahidi wafike mapema uwanja wa ndege ikiwezekana masaa saba kabla ya safari zao na gharama hizi za kipimo cha pili ni sawa na ile ya kipimo cha kwanza." Alisema Kakuru.
Aidha katika kuhakikisha ndege hizo za Falme za Kiarabu zinaendelea na safari zake hapa nchini, Meneja wa ndege za Emirates Tanzania uwanja wa ndege wa Terminal 3, Bw. Aboubakar Juma amemhakikishia Mganga mkuu wa Serikali kuwa, Emirates itaendelea na safari zake ambapo kwa sasa wanasubiria kukamilika kwa taratibu ndani ya uwanja huo.
"Tunapenda kuujulisha umma kwamba, kutokana na matakwa mapya ambavyo vilevile yamekuja ghafla kutoka Falme za Kiarabu kwa wasafiri kutoka Tanzania wanaokwenda Dubai, wataitajika kupima mara mbili, ikiwemo PCR covid test saa sita kabla ya safari.
Aidha, amesema baada ya taratibu, watatumiwa majibu yao kupitia simu zao kwa kupitia mtandao wa WhatsApp ama email kisha taratibu zingine na safari.
Wasafiri wanatakiwa kufanya miahadi ya safari zao 'booking' kupitia mtandaoni katika; na kufanya malipo na kisha kuchagua kituo cha kupima na kupata cheti ambacho kinakuwa tayari ndani ya masaa 48.
Nae Kaimu Mkurugenzi wa mahabara kuu ya taifa, amewaomba wasafiri ambao wanatakiwa kupima uwanja wa ndege ni wale tu wanaokwenda ama kupitia Dubai pekee na wale wengine watatumia utaratibu wao wa kawaida.
0 Comments