New Content Item (1)

Mradi wa Cap TB wa kupambana na ugonjwa wa kifua kikuu kwa watoto katika mikoa ya Tabora na Singida umebaini watoto wenye ugonjwa huo  kutoka 335 mwaka 2017 hadi watoto 1,852 mwaka 2021.

 Akizungumza wakati wa kuhitimisha mradi huo ulioanza mwaka 2017 mkurugenzi wa ufundi wa shirika lisilo la kiserikali la Egpaf lililokuwa na mradi huo, Dk Chrispine Kimario amesema watoto hao walipatikana baada ya kufuatwa na kuangaliwa afya zao na mara moja kuanzishiwa matibabu.

Ameeleza kuwa hata idadi ya watoto walioanzishiwa matibabu baada ya kugundulika kuwa na ugonjwa huo nayo imeongezeka kutoka watoto 303 mwaka 2017 hadi watoto 1,851 katika vituo vilivyofikiwa na mradi.

Mradi wa Cap TB katika mikoa ya Tabora na Singida imehusisha halmashauri 12 na kufikia vituo vya kutolea huduma za afya 45 ikiwemo 17 mkoa wa Tabora na 28 Mkoa wa Singida.

DK Kimario ameongeza kuwa kwa kutumia utaratibu wa ufuatiliaji wa kaya zenye wagonjwa wa kifua kikuu, mradi umefanikiwa kufikia kaya 343 ambapo jumla ya watoto 119 waliibuliwa kwa kukutwa na ugonjwa huo  na kupewa matibabu stahiki huku watoto 1,264 chini ya miaka mitano ambao hawakukutwa na ugonjwa huo wakipatiwa tiba ya kinga ya kifua kikuu.

"Mradi huu ukiwa unahitimishwa ujuzi walioachiwa watoa huduma,utaendelea kuwa nguzo muhimu katika utambuzi wa watoto wenye kifua kikuu hasa wale walio chini ya umri wa miaka mitano ambao hawawezi kutoa makohozi kwa njia ya kukohoa kawaida," amesema.

Akihitimisha mradi huo uliofadhiliwa na Unitaid meneja wa mpango wa Taifa wa kidhibiti kifua kikuu na ukoma kutoka Wizara ya Afya,Dk Riziki Kisonga ameupongeza mradi huo kuwa umekuwa na manufaa makubwa katika kuokoa maisha ya watoto na kutaka jitihada zielekezwe kwa makundi maalum na watoto hasa chini ya miaka mitano.

Amesema mradi umeonesha mbinu za kupunguza madhara yatokanayo na kifua kikuu na mikoa ya Singida na Tabora imefanya vizuri katika kuwabaini watoto wenye ugonjwa huo.