Na Said Mwishehe,Michuzi TV
SHIRIKA la Maendeleo la Japan( JICA)kwa kushirikiana na WaterAid Tanzania wanatarajia kutumia zaidi ya bilioni 3.6 kwa ajili ya kukusanya taarifa katika shule za msingi 30 na vituo vya afya 15 katika Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani ambazo zitasaidia kukuza uelewa wa umuhimu wa unawaji mikono na usafi ili kukabilianana magonjwa hatarishi.
Kwa mujibu wa Shirika hilo mradi huo ulianza rasmi Oktoba 2021 na wanategemea udumu kwa kipindi cha miezi 26 hafi ifikapo Novemba 2023 na kiasi hicho cha fedha kitatumika katika mradi huo katika shughuli mbalimbali mpaka pale utakapokamilika na kukabidhiwa kwa wananchi.
Akizungumza leo Desemba 2,2021 wilayani Kisarawe mkoani Pwani wakati wa uzinduzi rasmi wa mradi utakaogusa shule 30 na vituo vya afya 15 katika wilaya hiyo ,Mkurugenzi Mkaazi wa Shirika la WaterAid Anna Tenga Mzinga ametumia nafasi hiyo kuipongeza Serikali na kwamba wanatambua kuwa usafi wa mikono na mazingira kwa ujumla ni muhimu kwa usalama wa afya za wanajamii ili kukabiliana na magonjwa yatokanayo na uchafu katika nchi ya Tanzania na duniani kote.
"Hasa katika kipindi hiki tunapopambana na janga kubwa la ugonjwa wa UVIKO-19 .Takwimu zinaonesha kuwa asilimia 30 ya magonjwa ya kuhara yanaweza kuzuilika kwa unawaji wa mikono ulio sahihi, katika kuendeleza jitihada za Serikali katika kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma za maji safi,elimu pevu ya usafi binafsi na mazingira , JICA kwa kushirikiana na Shirika la WaterAid Tanzania tumeona umuhimu wa kukusanya taarifa katika shule na vituo vya afya ambazo zitasaidia kukuza uelewa,"amesema Mzinga.
Ameongeza bado kuna uhitaji mkubwa wa kuendelea kuhamasisha ili ifikapo 2030 kila Mtanzania apate huduma za maji safi,elimu pevu ya usafi binafsi na mazingira."Kipekee natoa shukrani zangu za dhati kabisa kwa niaba ya WaterAid Tanzania kwa kushirikiana na JICA kwa kuona umuhimu wa kufadhili mradi huu katika halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe ili kuhakikisha ubadilishaji tabia endelevu wa masuala ya usafi katika shule na vituo vya afya.
Mzinga ameahidi kuendelea kushirikiana na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya usimamizi thabiti wa Rais Samia Suluhu Hassan kupitia mradi huo na iliyo katika maeneo mengine nchini Tanzania.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Nickson Nickson Simon amesema mradi huo umekuja wakati muafaka na kwamba wanatambua umuhimu wa jamii kupewa elimu kuhusu usafi wa mazingira na binafsi ukiwemo wa unawaji mikono huku akifafanua kubadilisha tabia ni jambo linalohitaji msukumo mkubwa."Tunaweza kubadili jengo ndani ya muda mfupi lakini ni ngumu kubadilisha tabia, tunawashukuru JICA na WaterAid kwa kutuletea mradi huu Kisarawe.
Amefafanua elimu ya unawaji mikono inahitajika pia kwani huko nyuma aliwahi kupata elimu,unaweza kuona unanawa mikono lakini kumbe unaosha vidole tu,hivyo kuwajengea uelewa wananchi kutambua ni jinsi gani unatakiwa kuwa mikono ni jambo nzuri.
Wakati huo huo Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe Chichi Bella ameshukuru kwa kuupata mradi huo wa usafi wa binafsi na usafi wa mazingira na kwamba watatoa kila aina ya ushirikiano kuufanikisha mradi huo na kwamba watautekeleza kwa kiwango cha juu na baada ya mradi huo kuisha 2023 ,JICA na WaterAid watatamani kuwapatia mradi mwingine.
0 Comments